Rais wa Marekani Barack Obama ameapa kulizunguka bunge na kuchukua hatua
kivyake ili kuwaimarisha watu wa tabaka la kati, akionyesha kukatishwa
kwake tamaa na kasi ndogo ya kutunga sheria kwa upande wa bunge hilo.
Rais Obama akitoa hotuba yake kuhusu hali ya taifa.
Katika ujumbe wake kwa bunge la Congress kupitia hotuba yake ya kila
mwaka kwa taifa, Obama aliahidi kuchukua hatua kukabiliana na ongezeko
la ukosefu wa usawa, hata ikimbidi kufanya hivyo bila uungwaji mkono wa
bunge, huku akiwataka wabunge kuweka pembeni tofauti za kisiasa na
kufanya kazi kwa maslahi ya raia na kulipeleka mbele taifa hilo.
Rais Obama alisema nchi hiyo laazima iondokane na mawazo ya kupigana
vita mara kwa mara ili kutoa fursa kwa diplomasia kutatua matatizo sugu
ya ulimwengu, kama vile mgogoro wa nyukilia wa Iran. Obama pia alitoa
wito wa kuchukuliwa hatua za dhati kuufufua uchumi wa Marekani, na
kukabiliana na ukosefu wa usawa na kupanua fursa kwa raia wote wa taifa
hilo.
Hadhira ikimsikiliza Obama katika ukumbi wa bunge la Congress.
Mwaka wa kuchukuwa hatua
"Tuufanye mwaka huu kuwa mwaka wa kuchukuwa hatua. Hilo ndilo Wamarekani
wengi wanalolitaka. Kwetu sote katika jumba hili, kuyajali maisha,
matumaini na matarajio yao, na ninachoamini kinawaunganisha watu wa
taifa hili bila kujali rangi, dini au chama wanakotoka, wadogo kwa
wakubwa, matajiri na maskini, ni imani yao ya juu katika fursa kwa
wote," alisema rais Obama aliekuwa akishangiliwa mara kwa mara na
hadhira yake.
Comments