SOMA MAAMUZI YA KAMATI KUU YA CHADEMA YA KUWAVUA UANACHAMA DKT.KITILA MKUMBO NA SAMSON MWIGAMBA YALIYOTOLEWA LEO NA KATIBU MKUU WA CHADEMA DR WILBROD SLAA MBELE YA WAANDISHI WA HABARI
Katibu Mkuu wa Chadema Dr Wilbrod Slaa
---
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
UTANGULIZI
Kamati
Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ilikaa kikao cha
dharura ili kupokea, kujadili na kuamua juu ya utetezi wa mashtaka ya
ukiukaji wa Katiba, Kanuni na Mwongozo wa Chama yaliyokuwa yanawakabili
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zitto Zuberi Kabwe, aliyekuwa mjumbe wa
Kamati Kuu Dr. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa
Arusha Samson Mwigamba.
Kikao hicho cha dharura kilifanyika Dar es Salaam kati ya tarehe 3-4
Januari, 2014. Kabla ya kuanza kwa kikao, Kamati Kuu ilipokea taarifa
kwamba Zitto Zuberi Kabwe amefungua mashtaka dhidi ya CHADEMA katika
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam. Aidha, Kamati Kuu
ilijulishwa kwamba Mahakama Kuu imetoa amri ya zuio la muda ya kuizuia
Kamati Kuu au chombo kingine cha Chama kutokukaa, kujadili na kuamua
suala la uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe. Kutokana na amri hiyo ya
Mahakama Kuu, Kamati Kuu haikujadili na kuamua juu ya mashtaka dhidi
yake.
MASHTAKA
Watuhumiwa
wote watatu walishtakiwa jumla ya mashtaka 11 yanayohusu ukiukaji wa
vifungu mbali mbali vya Katiba ya Chama, Kanuni za Uendeshaji Kazi za
Chama, Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa
Chama na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi
Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali. Mashtaka yote yalitokana na
watuhumiwa kuandaa kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko, 2013 kama
ifuatavyo:
1. Kukashifu Viongozi Wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa Mh. Freeman A. Mbowe, na Katibu Mkuu Dr. Wilbrod P. Slaa;
2. Kutokuwa
wakweli na wawazi kwa kushirikiana na vikundi vya majungu kwa kuanzisha
na kuratibu mtandao wa siri ulioitwa ‘Mtandao wa Ushindi’ nje ya
utaratibu wa Chama ili kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya
Mwenyekiti wa Chama Taifa;
3. Kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa Chama na bila kupitia vikao halali vya Chama;
4. Kujihusisha
na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini na ukanda vyenye makusudi
ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii;
5. Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa Chama na wanachama wake;
6. Kuandaa
na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa
bila kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa Mwongozo wa Chama;
7. Kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania uongozi ndani ya Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
8. Kuwachafua viongozi na wanachama wenye nia au kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
9. Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa Chama;
10. Kukashifu Chama na viongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge; na
11. Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge.
UTETEZI WA WATUHUMIWA
Watuhumiwa
wote walijitetea kwa maandishi. Zaidi ya utetezi huo wa maandishi, Dr.
Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba waliitikia wito wa Kamati Kuu wa
kujitetea kwa mdomo mbele yake.
Hata hivyo, siku ya utetezi wao, ni Dr.
Kitila Mkumbo peke yake aliyejitokeza kwenye Kamati Kuu na kujitetea kwa
mdomo. Katika utetezi wake wa maandishi, licha ya kukiri kushiriki
katika maandalizi ya kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013, Dr.
Kitila Mkumbo – kama ilivyokuwa kwa Samson Mwigamba – alikanusha na
kukataa tuhuma zote za kukiuka Katiba ya Chama, Kanuni zake na Mwongozo
wa Chama.
Kwa maneno yake mwenyewe, Dr. Mkumbo alikanusha “kila tuhuma
mojamoja na kwa ujumla wake dhidi yake”, na kwamba mashtaka hayo sio
ya kweli na hakuvunja Katiba, Kanuni wala Mwongozo wa Chama.
Aidha,
licha ya kukiri kwake katika kikao cha Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana
kwamba walioshiriki kuandaa Mkakati huo ni pamoja na mtu anayejulikana
kama M2, mara hii Dr. Kitila Mkumbo aliiambia Kamati Kuu kwamba “waraka
husika ulikuwa ni wa siri na haukuwahi kusambazwa wala kushirikisha …
wanachama au viongozi wa CHADEMA isipokuwa mimi binafsi na Samson
Mwigamba….” Vile vile, ijapokuwa katika Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana
Dr. Mkumbo alidai kutokumfahamu kabisa M2, mara hii aliiambia Kamati
Kuu kwamba anamfahamu fika M2 lakini hayuko tayari kumtaja mbele ya
Kamati Kuu hadi atakapowasiliana naye!
USHIRIKI WA ZITTO ZUBERI KABWE KATIKA MKAKATI WA MABADILIKO
Itakumbukwa
kwamba katika kikao cha Novemba 2013, Dr. Kitila Mkumbo na Zitto Zuberi
Kabwe walikataa kata kata kuhusika kwa Zitto Zuberi Kabwe katika
maandalizi ya Mkakati wa Mabadiliko.
Aidha, Zitto Zuberi Kabwe alidai
mbele ya Kamati Kuu kwamba alikuwa ameusikia Mkakati huo kwa mara ya
kwanza kwenye Kamati Kuu, na amerudia kauli hiyo mara nyingi na
hadharani tangu avuliwe nafasi zake za uongozi. Hata hivyo, wakati wa
mahojiano na wajumbe wa Kamati Kuu, Dr. Kitila Mkumbo alikiri kwamba
yeye na waandishi wenzake wa Mkakati walimpa Zitto Zuberi Kabwe briefing
juu ya Mkakati na kwamba alikuwa anaufahamu.
Ukweli huu pia
umethibitishwa na mawasiliano ya baruapepe iliyotumwa na Zitto Zuberi
Kabwe mwenyewe kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA Mpya 2014’ tarehe 27 Oktoba,
2013, karibu mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Novemba
iliyowavua madaraka.
Zaidi
ya hayo, baada ya kuonyeshwa waraka wa Chama juu ya mabadiliko ya
Katiba ya Chama uliotumwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama wakati
huo Shaibu Akwilombe Julai 2006 unaothibitisha kwamba mabadiliko ya
Katiba yaliyoondoa ukomo wa uongozi yalifanywa kwa uwazi na kwa
kushirikisha ngazi zote za Chama, Dr. Kitila Mkumbo alikataa kata kata
kujadili suala hilo kwa madai kwamba tayari walishapeleka malalamiko yao
kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Kuhusu
tuhuma zao kwamba kuna ufisadi na ubadhirifu wa fedha za Chama
unaofanywa na Mwenyekiti wa Chama, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha
Anthony Komu na kwamba taarifa za matumizi ya fedha ni siri ya viongozi
hao watatu, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa mbali mbali za fedha
zilizowasilishwa mbele ya vikao vya Kamati Kuu a Chama ambavyo yeye
mwenyewe na Zitto Zuberi Kabwe walishiriki kama wajumbe wa Kamati Kuu.
Aidha, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa za kibenki zinazoonyesha jinsi
michango ya Mzee Jaffer Sabodo na michango mingine ya watu binafsi
zilivyopokelewa na kutumiwa na taarifa zake kuwasilishwa kwenye vikao
vya Kamati Kuu walivyohudhuria yeye na Zitto Zuberi Kabwe.
Zaidi
ya hayo, Dr. Mkumbo alionyeshwa nyaraka za manunuzi ya vifaa vya Chama
kama vile vile pikipiki, kadi, bendera, n.k, na jinsi ambavyo uamuzi wa
manunuzi hayo yalifanywa na Kamati Kuu ambayo wao wenyewe ni wajumbe na
walihudhuria vikao husika. Vile vile, Dr. Mkumbo alionyeshwa ushahidi wa
maandishi kwamba Mwenyekiti wa Chama hakuhusika kwa namna yoyote ile
katika manunuzi hayo na hakuna karatasi yoyote inayoonyesha saini ya
Mwenyekiti katika manunuzi ya vifaa hivyo.
Aidha, Dr. Mkumbo hakuweza
kuthibitisha kwa namna yoyote kwamba CHADEMA ina mkataba wowote na watu
binafsi wanaouza vifaa vya uenezi vya Chama kwa vile Kamati Kuu ya Chama
katika vikao ambavyo vilihudhuriwa na Dr. Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe
ilikwisharuhusu wafanya biashara binafsi kuagiza vifaa hivyo na kuviuza
kwa wanachama wanaotaka kuvinunua. Kwenye yote haya, Dr. Kitila Mkumbo
hakuwa na lolote la maana la kuiambia Kamati Kuu.
MAAMUZI YA KAMATI KUU
Baada
ya kusikiliza utetezi wa Dr. Kitila Mkumbo na baada ya kumhoji kwa
kirefu, Kamati Kuu imeridhika bila mashaka yoyote kwamba Mkakati wa
Mabadiliko 2013 haukuwa na lengo la kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa
nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama peke yake. Mkakati huo ulikuwa
na malengo makubwa zaidi ya kukibomoa Chama kwa kukichafua kwa wananchi
na kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo za
ufisadi. Hii ni kwa sababu, kwa maoni ya Kamati Kuu, Chama cha siasa
ambacho viongozi wake wa juu wanatuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi kuaminiwa
na wananchi kama tumaini lao la ukombozi.
Kamati
Kuu imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbali mbali zilizoandaliwa na
Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe ama na mawakala wake wakitumia vitambulisho
bandia katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba mkakati wa
kukibomoa Chama umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu.
Mkakati huo
ulihusisha pia hujuma dhidi ya Chama kwa kuwaengua wagombea wake katika
chaguzi mbali mbali kama ilivyotokea katika majimbo ya Mpanda Mashariki,
Musoma Vijijini na Singida Mjini ambapo Zitto Zuberi Kabwe alishiriki
moja kwa moja.
Kwa sababu zote hizo, Kamati Kuu imeazimia ifuatavyo:
1. Kwamba
kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba
wafukuzwe uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA); na
2. Kwamba,
kwa vile Zitto Zuberi Kabwe amekishtaki Chama kinyume na matakwa ya
Katiba ya Chama na Kanuni zake, na kwa vile Mahakama Kuu imeamuru vikao
vyote vya Chama visijadili wala kuamua suala lolote linalohusu uanachama
wa Zitto Zuberi Kabwe, viongozi wa ngazi zote za Chama, wanachama,
washabiki na wapenzi wa CHADEMA popote walipo katika nchi yetu na nje ya
Tanzania wasishiriki wala kusaidia kwa namna yoyote mikutano yoyote ya
nje au ya ndani au shughuli nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na
Zitto Zuberi Kabwe na mawakala wake kwa jina la CHADEMA.
——————————–
Dr. Wilbrod P. Slaa
KATIBU MKUU
Comments