Na Hassan Hamad OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema
Zanzibar inahitaji kujipanga ili kulinda mafanikio yaliyopatikana
kutokana na mradi wa kutokomeza malaria Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na watendaji wa kitengo cha malaria
Mwanakwerekwe wakati wa ziara yake katika kitengo hicho. Kushoto ni
msaidizi meneja wa kitengo cha Malaria Zanzibar Bw. Mwinyi Msellem.
(picha, Salmin Said, OMKR)
Amesema mafanikio yalipatikana yameiletea sifa kubwa Zanzibar, hali inayopelekea kuigwa na nchi nyengine duniani.
Maalim Seif ameeleza hayo katika kitengo cha kudhibiti malaria Zanzibar
huko Mwanakwerekwe, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya
kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya kwa upande wa Unguja.
Amesema mafanikio hayo yanapaswa kulindwa na kuhakikisha kuwa malengo
yaliyotarajiwa ya kuifanya Zanzibar bila ya kuwa na Malaria yanafikiwa
kwa wakati.
“Nataka hapa tulipofika tusirudi nyuma, serikali kwa upande wake
itajitahidi kuweka mikakati ili kuona kuona kuwa tunasonga mbele hadi
kutimiza malengo yetu”, alisistiza Maalim Seif.
Kwa upande wake msaidizi meneja wa kitengo cha Malaria Zanzibar Bw.
Mwinyi Msellem amesema Zanzibar imepata mafanikio makubwa ya kupambana
na malaria katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ambapo kwa sasa
ugonjwa huo upo chini ya asilimia moja kutoka asilimia 45 mwaka 2001.
Amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na mchango mkubwa wa
washirika wa maendeleo, pamoja na mipango imara ya taasisi hiyo ikiwemo
ugawaji wa vyandarua vyenye dawa, utiaji wa dawa za kuulia mbu wa
malaria majumbani pamoja kufuatilia kwa karibu wagonjwa wanaougua
malaria ili kuwapatia matibabu yanayostahiki.
Comments