Ruto anataka asilimia 50 ya nyadhifa hizo na amemwambia Kenyatta kwamba
atagawa nyadhifa zilizosalia na vyama vingine katika muungano huo kama
vile New Ford Kenya ya Eugene Wamalwa na Narc ya Charity Ngilu.
MGOMBEA Urais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amekuwa katika ziara zisizokoma
za nchi za Afrika Mashariki kwa lengo la kutafuta uungwaji mkono wa
marais wa nchi hizo.
Tayari amekutana na kufanya mashauriano na viongozi wa Tanzania,
Burundi, Sudan Kusini miongoni mwa wengine, na bado anaendelea na ziara
hizo.
Huku nyumbani, baadhi ya viongozi na wagombea wa urais kama vile Naibu
Waziri Mkuu, Musalia Mudavadi na Martha Karua wanatoa onyo kali na
ushauri kwa Wakenya wasidhubutu kuwachagua washukiwa hao wasije
wakajuta.
Mudavadi anasema kwamba Wakenya wakifanya makosa ya kuwapa Kenyatta na
William Ruto jukumu la kuwaongoza, nchi itakuwa katika mashaka makubwa
katika nyanja za kiuchumi na kisiasa ulimwenguni. Kiongozi huyu hapo
awali alikuwa akiunga mkono wawili hao na hata kuwaambia Wakenya kuwa
mzigo wanaobeba viongozi hao katika Mahakama Kuu ya Kimataifa ya ICC
huko The Hague, Uholanzi, ni mzigo wa Wakenya wote.
Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka kwa kuwa bado anatarajia kwamba kuna
uwezekano wa kuwa katika muungano na washukiwa hao, haswa Ruto, hataki
kamwe kugusia suala hili. Juzi, katika mkutano wa kisiasa, aliukejeli
muungano ambao sasa unayumbayumba kati ya Kenyatta na Ruto. Mazungumzo
ya muungano kati ya viongozi hao wawili yamepigwa na dhoruba kali kwa
sababu hawajakubaliana kuhusu nyadhifa za mawaziri na maspika wa Bunge
na Seneti.
Comments