Bwalya |
KALUSHA BWALYA:
SAHAU kuhusu Zambia iliyochukua Kombe a Challenge mwaka
2006, wakati huo imekwishajitoa katika nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya
Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na kuingia nchi za Kusini mwa Afrika
(COSAFA).
Zambia iliyotikisa katika soka ya Afrika Mashariki na kati
ni ile iliyokuwa ikiitwa KK Eleven kuanzia miaka ya 1970 hadi 1990 mwanzoni,
kabla ya ajali ya ndege iliyoua nyota wa kikosi hicho pwani ya Gabon mwaka 1993.
Kalusha Bwalya alikuwa katika orodha ya wachezaji
waliotakiwa kuingia kwenye ndege iliyopata ajali, lakini bahati nzuri kwake
alisema atatokea kwenye klabu yake moja kwa moja Ulaya kwenda Tunisia, hivyo
akanusurika.
Katika historia yake ya ushiriki wa Challenge, KK Eleven
ilibeba taji hilo mwaka 1984 na 1991 ambao, Kalusha Bwalya aliungana na Majid
Musisi katika ufungaji bora, kila mmoja akifunga mabao yake matatu.
Challenge ya mwisho kwa Bwalya ilikuwa mwaka 1992 mjini
Mwanza, alipoiongoza Zambia hadi Nusu Fainali ilipotolewa na Uganda kwa penalti
4-2, Uwanja wa CCM Kirumba kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.
Huwezi kuizungumzia historia ya Challenge bila ya kumtaja
Bwalya, aliyezaliwa Agosti 16, mwaka 1963 mjini Mufulira, kwani enzi zake
alikuwa mkali haswa.
Huyo ni mchezaji aliyeichezea Zambia mechi nyingi zaidi na
kuifungia mabao mengi zaidi pia kuliko mchezaji yoyote hadi sasa. Ndiye
mchezaji babu kubwa zaidi kuwahi kutokea katika ardhi ya Zambia. Unamzungumzia
Mwanasoka Bora wa Afrika mwaka 1988, ambaye mwaka 1996 aliingia kwenye
kinyang’anyiro cha tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia, ambayo ilichukuliwa na
Mwafrika mwenzake, George Weah.
Omondi Philip |
PHILIP OMONDI:
UGANDA ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Challenge,
wakiwa wamebeba Kombe hilo mara 12 (1973, 1976, 1977, 1989, 1990, 1992, 1996, 2000, 2003,
2008, 2009 na 2011).
Wapo wachezaji wawili ambao huwezi kuwatenganisha na
mafanikio ya The Cranes katika Challenge. Akina nani hao?
Wote hawa wamekwishatangulia mbale ya haki hivi sasa, Philip
Omondi na Majjid Musisi.
Phillip Omondi aliyezaliwa mwaka 1957 na kufariki dunia Aprili
21, mwaka 1999 huyu alikuwa mtu hatari sana enzi zake na waliobahatika kumuona
wanaweza kukiri juu ya hilo.
Omondi aliyechezea klabu ya Kampala City Council FC kuanzia
mwaka 1973 hadi 1979, alipotimkia Sharjah ya Falme za Kiarabu (UAE) alikuwa
shukaa wa Uganda hadi kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Omondi aliichezea The Cranes katika fainali za Afrika miaka
ya 1974, 1976 na za 1978, ambazo pamoja na kuifikisha Cranes fainali, pia
aliibuka mfungaji bora.
Kwenye Challenge, Omondi aliisaidia mno Uganda kutwaa mataji
ya mwaka 1973 na 1977.
Katika fainali za mwaka 1978, mkali wa mabao wa zamani wa
Uganda, Phillip Omondi aliungana na Opoku Afriyie na Segun Odegbami katika
ufungaji bora, kila mmoja akipachika nyavuni mabao matatu. Leo Omondi hayupo
duniani, lakini huwezi kuzungumzia historia ya Challenge bila kumtaja yeye.
Musisi |
MAJID MUSISI:
NI kweli, Philipo Omondi alikuwa noma enzi zake, lakini
unaweza kusema nini kuhusu Majid Musisi Mukiibi?
Mshambuliaji huyo aliyezaliwa Septemba 15, mwaka 1967 kabla
ya kufariki dunia Decemba 13, mwaka 2005 vyombo vya habari Uganda vimechekecha
vikaamua kuweka bayana, huyo ndiye mchezaji bora zaidi kihistoria kuwahi
kutokea nchini humo.
Musisi, ambaye ni mchezaji wa kwanza wa Uganda kucheza soka
ya kulipwa Ulaya, alikuwa ana majina mawili maarufu ya utani enzi zake, ambayo
ni Tyson na Magic. Tyson kwa sababu alikuwa mkorofi na Magic ni kwamba soka
yake iliitwa ya miujiza.
Huyo aliisaidia The Cranes kutwaa Kombe la Challenge katika
miaka ya 1989 na 1990. Mfumo wa maisha ya kuendekeza pombe, ulimfanya
afananishwe na magwiji wa soka duniani akina George Best, Eric Cantona au Paul
Gascoigne ‘Gazza’.
Musisi alikuwa ana utajiri miguuni mwake na mabeki kwa
pamoja na makipa walikuwa wanamheshimu sana mtu huyo. Alikuwa hashindwi kufanya
jambo anapoamua kufanya kwa juhudi zake zote.
Umaarufu wake uliwavutia vijana wengi kucheza soka Uganda na
Afrika Mashariki kwa ujumla. Jamaa alikuwa anaijua soka.
Nteze John |
NTEZE JOHN:
WENGINE wanaweza kujiuliza kwa nini siyo Sunday Manara ama
Zamoyoni Mogella, Peter Tino au Edibily Lunyamila, lakini jibu ni kwamba, wote
hao hawafui dafu mbele ya Nteze John Lungu kwa kufanya vitu vikubwa kwenye
Kombe la Challenge.
Haimaanishi Nteze alikuwa anawazidi kisoka akina Abdallah
Kibadeni, Mogella, Lunyamila, Said Mwamba Kizota na wengine waliowahi kuwika
katika soka ya Tanzania, la hasha- ila Nteze aling’ara zaidi yao kwenye
michuano hiyo.
Huyo ndiye aliyekuwa shujaa wetu wakati tunachukua taji la
pili la michuano hiyo, mwaka 1994 mjini Nairobi, Kenya.
Mabao yake manne aliyofunga katika Kundi A, kwenye michuano
hiyo yaliifanya Tanzania Bara iongoze kundi hilo kwa pointi tisa ilizokusanya
kutoka na kushinda mechi zote za kundi lake, Nteze akifunga katika kila mechi.
Novemba 29, Tanzania ikiitandika Somalia mabao 4-0, Nteze
alifunga mabao mawili katika dakika za 11 na 84, mengine yakifungwa na George
Masatu dakika ya 67 na Madaraka Suleiman dakika ya 74.
Siku mbili baadaye Nteze alifunga bao pekee la ushindi
dakika ya 57, Bara ikiwafunga wenyeji Kenya 1-0, wakati Desemba 3, Bara
ikiichapa Djibouti 3-0, Nteze alifunga la tatu dakika ya 75, baada ya Edward
Chumila (sasa marehemu) kufunga dakika ya pili na Clement Kahabuka dakika ya
30.
Nteze hakufunga katika mechi mbili zilizofuata, Nusu Fainali
dhidi ya Eritrea, bao pekee la Said Mwamba ‘Kizota’ dakika ya saba likiipa Bara
ushindi wa 1-0 na fainali, ambayo baada ya sare ya 2-2 ndani ya dakika 120
dhidi ya Uganda, Bara ilifanikiwa kutwaa Kombe kwa mikwaju ya penalti 4-3.
Ilikuwa ni Desemba 10, wakati mabao ya Stars yalipotiwa
kimiani na Juma Amir Maftah dakika ya 14 na Kizota dakika ya 40 wakati Iddi
Batambuze aliifungia Uganda dakika ya 47 kabla ya George Ssemogerere dakika ya
88 kusawazisha.
Nteze aliibuka pia mfungaji bora wa michuano hiyo kwa mabao
yake manne na kutwaa Kiatu cha Dhahabu.
Oliech |
DENNIS OLIECH:
WAMETOKEA wanasoka wengi Kenya ambao waling’ara kwenye
Challenge, lakini kama ilivyo kwa wachezaji wa Tanzania unahitajika utulivu wa
hali ya juu, ili kumtaja mmoja ambaye daima anastahili kukumbukwa katika
historia ya michuano hiyo.
Mfungaji wa bao la tatu na la ushindi katika dakika ya 72 ya
fainali ya Kombe la Challenge Desemba 14, mwaka 2002 Uwanja wa CCM Kirumba mjini
Mwanza, Tanzania Bara ikilala 3-2 na kupoteza matumaini ya kutwaa taji hilo kwa
mara ya tatu.
Nani zaidi ya Dennis Oliech. Na kwa nini asahaulike mtu huyo
siyo tu kwa kuwakomoa wenyeji na kuwapokonya tonge mdomoni, bali soka yake
iliyomuuza Ulaya baadaye.
Siku hiyo, Emmanuel Gabriel alitangulia kuifungia Bara
dakika ya 28, kabla ya Paul Oyuga kusawazisha dakika ya 30 na Mecky Mexime kufunga
la pili kwa penalti dakika ya 59 na John Barasa kuisawazishia Harambee Stars
dakika ya 70 na Oliech kupiga la ushindi dakika ya 72.
Oliech alikuwa mfungaji bora katika fainali hizo kutokana na
mabao yake matano, akiwa ana umri wa miaka 17 tu wakati huo.
Oliech alizaliwa Februari 2, mwaka 1985, baada ya kung’ara
kwenye fainali hizo, mwaka 2003 alinunuliwa na Al-Arabi ya Qatar hadi mwaka
2005, aliposaini mkataba wa miaka minne na
FC Nantes ya Ufaransa na kuanza safari yake kuogelea kwenye bwala la
fedha Ulaya na sasa anachezea Auxerre.
Aliiwezesha Kenya kukata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika mwaka 2004 na alicheza vizuri kwenye fainali hizo nchini
Tunisia na mwaka huo huo akatabiriwa kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari
baadaye duniani, akiwekwa katika orodha moja na Wayne Rooney wa Manchester
United. Oliech kwa sasa ameipa kisogo michuano ya Challenge, ingawa bado anaichezea
Harambee Stars katika michuano mikubwa, ila Challenge ndio iliyomtoa.Source Bin Zubeiry.
Comments