MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeifilisi akaunti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuchukua sh. milioni 300.
TRA imechukua fedha hizo katika akaunti ya TFF iliyopo katika benki ya NMB.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Sunday Kayuni alisema jana kuwa, TRA imechukua fedha hizo ili kufidia deni lililotokana na malimbikizo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inayotokana na mishahara ya makocha wa timu ya taifa.
Kayuni alisema kuwa, TRA inadai sh. 157, 407, 968 za VAT za mishahara ya aliyekuwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo na msaidizi wake, Itamar Amorin, Jan Poulsen, Kim Poulsen na Jacob Mitchelsen.
Alisema kwa mujibu wa TRA, mishahara ya makocha hao ilitakiwa kukatwa VAT, lakini kwa kuwa serikali ndiyo iliyokuwa ikilipa mishahara hiyo, hakuna kodi iliyokatwa.
Kayuni alidai kuwa, TRA imeionea TFF kuchukua fedha hizo, ambazo zilitolewa na mdhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom.
Alisema serikali ilipaswa kulipa kodi hiyo kwa kuwa ndiyo inayolipa mishahara ya makocha wa timu za taifa, na siyo TFF, ingawa shirikisho hilo ndilo mwajiri wao.
"Kuchukuliwa fedha hizo kutasababisha mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania Bara kusuasua, hatutakuwa na fedha za kuzilipa klabu kwa maandalizi ya mechi zake,"alisema Kayuni.
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema TFF inawasiliana na serikali kuijulisha hatua ya TRA, ingawa mara kadhaa waliwahi kuzungumza nao kuhusiana na jinsi ya kulipa deni hilo.Inatoka kwa mdau.
Comments