Na Mwandishi Wetu
VYOMBO vya habari nchini Misri vimeahidi kutangaza vivutio mbalimbali
vya utalii vilivyopo nchini katika kuhakikisha Tanzania inapata watalii
wengi zaidi jambo litakaloendelea kudumisha mahusiano mema yaliyopo kati
ya nchi hizo.
Marwa
Tawfik (Kulia) mmoja wa wajumbe waliowakilisha vyombo vya habari nchini
Misri kuja Tanzania kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii akifafanua
jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na waandishi wa
habari (hawapo pichani) juu ya kile walichojionea walipofanya ziara
katika vivutio mbalimbali vya utalii Tanzania Bara na Zanzibar.Wengine
ni baadhi ya wawakilishi kutoka Misri.
Hayo yalisema Dar es Salaam juzi na mmoja wa wawakilishi wa vyombo vya
habari nchini Misri, Marwa Tawfik alipozungumzia ziara waliyofanya
katika vivutio vya utalii nchini ambapo waliahidi kutumia vyombo vyao
kutangaza walivyoviona.
Ujumbe wa watu sita uliowakilisha vyombo mbalimbali vya habari nchini
Misri yakiwemo magazeti na televisheni chini ya Ofisa wa Ubalozi wa
Tanzania nchini humo Jestas Nyamanga walifanya ziara ya siku tano nchini
kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii Tanzania Bara na Visiwani
chini ya uratibu wa Bodi ya Utalii nchini (TTB).
Alisema wanaporudi nchini kwao watakaa na uongozi wa vyombo vyao na
kuangalia jinsi ya kupata vipindi maalumu katika televisheni na makala
katika magazeti jambo litakalowezesha taarifa za utalii za Tanzania
kuwafikia watu wengi zaidi nchini mwao na nchi nyingine za ukanda huo.
Tawfik alisema ana imani ziara hiyo pamoja na kazi watakayoifanya ya
kuvitangaza vivutio husika itasaidia Tanzania kupata watalii wengi zaidi
kutoka nchini mwao na katika nchi za ukanda wa kiarabu. “Tumeona
utajiri wa asili wa ajabu uliopo Tanzania,sisi tunaahidi kutumia vyombo
vyetu kutangaza vivutio hivi katika kuhakikisha watu wengi zaidi
wanahamasika kuja Tanzania na hatimaye kuwaongezea pato lenu kupitia
utalii,” alisema Tawfik.
Comments