Hanoi,Vietnam 23.11.2012
ZANZIBAR na Vietnam zimekubaliana kuimarisha uhusiano na ushirikiano
katika kukuza sekta za maendeleo na uchumi huku Vietnam ikiahidi kuiunga
mkono Zanzibar katika kuhakikisha inafikia malengo yake iliyojiwekea
katika kuimarisha sekta za maendeleo na uchumi .
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed shein, wakaribishwa katika Ikulu ya
Vietnam,alipofika kwa mazungumzo na Makamo wa Rais wa Vietnam Bibi,
Nguyen Thi Doan,akiwa na ujumbe wake katika ziara rasmi ya Kiserikali
nchini humo ya wiki moja. [Picha na Ramadhan Othman Vietnam.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali
Mohamed Shein alisema kuwa ipo haja ya kuimarisha na kukuza uhusiano na
ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzaniaikiwemo Zanzibar na
Vietnam hasa katika sekta za maendeleo na uchumi.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa
Rais wa Vietman Mhe. Bi Nguyen Thi Doan huko katika ukumbi wa Ikulu ya
nchi hiyo mjini Hanoi.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar
ina mengi ya kujifunza kutoka Vietnam kutokana na nchi hiyo kupata
mafanikio makubwa katika uimarishaji wake wa uchumi na pamoja na sekta
za maendeleo.
Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya kuimarisha zaidi
ushirikiano huo kati ya Zazibar na Vietnam ni pamoja na sekta ya uvuvi,
kilimo, utalii, uimarishaji wananchi kiuchumi, biashara pamoja na sekta
nyenginezo.
Aidha, Dk. Shein amueleza Makamu huyo wa Rais kuwa Tanzania na Vietnam
zimekuwa na uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu tokea miaka ya 1960 na
zimeweza kuungana mkono katika mambo mbali mbali ya kimaendeleo,
kiuchumi na hata kisiasa.
Dk. Shein alimueleza kingozi huyo hatua zinazochukuliiwa na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo na uchumi na
mafanikio yaliofikiwa katika kutekeleza Dira ya 2020 pamoja na Mkakati
wa Kukuza Uchumi a Kupunguza Umasikini (MKUZA).
Kwa upande wa kilimo Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Tanzania imeweka mikakati maalum ya kuimarisha sekta ya kilimo ambapo kwa upande wa Zanzibar Serikali mechukua juhudi kubwa katika kuhakikisha sekta hiyo inapewa kipaumbele.
Comments