KIKOSI cha Simba kimewasili salama mjini Shinyanga na jana jioni kimeendelea na programu yao ya mazoezi kama kawaida wakijiwinda na mchezo wao wa ligi kuu utakaochezwa Alhamisi dhidi ya Mwadui.
Msafara wa Simba ulisafiri kwa ndege ya Shirika la ATCL alfajili ya leo Jumanne wakitokea Dar es Salaam.
Meneja wa kikosi hicho, Richard Robert amesema, timu imefika salama na maandalizi yao pamoja na mambo yote juu ya mchezo huo yanakwenda vizuri.
"Tunamshukuru Mungu tumefika salama hapa Shinyanga na jioni hii, tunatarajia kuendelea na programu yetu ya mazoezi kama kawaida kwa ajili ya maandalizi ya mechi yetu na Mwadui,"anasema Richard.
Simba ndiyo vinara wa ligi kuu, wanaongoza na pointi 41, wakifuatiwa na Yanga yenye 34, Azam watatu wana pointi 34, Singida United ya nne pointi 33 na Mtibwa Sugar wa tano na 27, watacheza mchezo huo Alhamisi na Ijumaa watarudi Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi mengine ya mechi yao ya kimataifa dhidi ya Gendarmarie ya Djibouti.
Watakwenda Djibouti Jumapili tayari kwa mchezo huo ambao ni wa awali wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika siku ya Jumanne.
Comments