Uongozi wa Simba umeweka wazi kuhusu hali ya mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi kuwa yupo fiti licha ya kushindwa kuendelea na mchezo wa juzi Jumatatu walioibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Mbao FC.
Mganda huyo ameonekana kuwa kwenye kiwango cha juu msimu huu, huku akifanikiwa kufunga mabao 16 ambayo yalifungwa na Simon Msuva msimu uliopita.
Okwi alitolewa nje ya uwanja dakika ya 76 kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Laudit Mavugo.
Simba waliweka taarifa kwenye ukurasa wao wa Istagram jana Jumanne ikieleza kwamba Okwi anaendelea vyema kutoka na majeraha aliyokuwa ameyapa wakati wakiisulubu Mbao FC.
Ratiba iliyotangazwa jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilieleza kwamba mchezo wa Simba na Stand United umerudishwa nyuma na utachezwa keshokutwa Ijumaa jijini Dar es Salaam.
Lengo la kutoa nafasi hiyo ni kuwapa muda Simba kupata nafasi ya kufanya maandalizi kuelekea mechi yake ya kimataifa na Waarabu itakayopigwa Machi 9 Uwanja wa Taifa.
Comments