Panya wakiwa shimoni.
Baadhi ya wakulima wa mashamba ya Miti katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa wamelalamikia uchomaji wa moto unaotokana na uwindaji wa Kitoweo aina ya panya na Sungura nyakati za kiangazi jambo linalowarudi nyuma kimaendeleo.
“Kipindi cha kiangazi, wawindaji huchoma moto mapori ili kuwinda panya. Kasumba hii ya kuchoma mapori imeanza miaka ya nyuma sana na imekuwa ikiwakatisha tamaa wakulima wa miti,” Mkulima wa miti Julius Maganga alisema hayo siku ya upandaji miti iliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Mpwapwa kilichopo ndani ya halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga.
Kufuatia kauli hiyo ilimlazimu mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wagabo kutoa agizo kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo huku akitaka sheria kutiliwa mkazo hasa kwa wale wanaokiuka kwa makusudi.
“Serikali kwa kushirikiana na wataalam wengine tunaangalia uwezekano wa kutumia sumu na kuwaua panya hao wakiwa huko huko msituni. Hii itasaidia kupunguza uharibifu wa misitu na mashamba ya miti kwa kiasi kikubwa,” alisema Wangabo.
Wilaya ya Sumbawanga inalengo la kupanda miti milioni 1.500,000 ambapo mpaka sasa jumla ya miti 830,000 imepandwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Comments