Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu(picha na mtandao)
Na Hellena Matale Dar es salaam
Serikali imesema kuwa inatarajia kutoa chanjo kwa wasichana 614,734 wenye umri wa miaka 14 nchini ili kuwakinga na saratani ya shingo ya kizazi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu mapema leo wakati akifungua mkutano wa wadau wa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa kati ya wagonjwa 100, wagonjwa 46 ni wa Saratani ya mlango wa kizazi na Saratani ya Matiti na vifo vitokanavyo na saratani kwa akina mama ni asilimia 50 ambapo chanzo ni saratani ya shingo ya kizazi na matiti.
Aidha amesema amesema kutokana na mazingira ya upatikanaji wa chanjo hiyo na gharama kuwa kubwa, wataitoa kwa wasichana wenye miaka 14 waliozaliwa kati ya mwaka 2003 na 2004.
Naye Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dafrossa Lyimo amewatoa hofu wananchi na kusisitiza juu ya umuhimu wa kinga kuliko tiba na kusema kuwa chanjo hiyo ni salama na imethibitishwa na shirika la Afya Duniani (WHO)na itatolewa na wahudumu wa afya waliopata mafunzo.
Chanjo hiyo itatolewa kwenye vituo vyote vya afya vya Serikali vipatavyo 7,000,mashuleni pamoja na huduma za afya za vikoba bila malipo
Comments