VINARA wa soka Tanzania Bara, Simba wameondoka nchini jana jioni kwenda
Djibouti, kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika
dhidi ya Gendarmerie Nationale utakaofanyika Februari 21.
Katika mchezo huo, Simba itamkosa nahodha wake John Bocco ambaye
alifunga mabao mawili katika mchezo wa kwanza uliomalizika kwa ushindi
wa 4-0, kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu wa kushoto aliyoyapata
kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC ambapo alishindwa kuendelea
na mchezo na kutolewa nje.
Akizungumza na gazeti hili Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pierre Lechantre,
alisema pamoja na kumkosa Bocco, lakini ana matumaini makubwa ya ushindi
kutokana na maandalizi waliyofanya pamoja na ari waliyokuwa nayo
wachezaji wake.
"Maandalizi yamekamilika, tumejipanga kuhakikisha tunacheza kwa nguvu
bila kujali kama tunaongoza kwa mabao manne najua mchezo utakuwa mgumu,
lakini lazima tusonge mbele kutokana na ubora wa timu yangu,” alisema
Lechantre.
Mfaransa huyo alisema amesafiri na kikosi cha wachezaji 19 wenye uhakika
wa kucheza na wa 20 ni Bocco ambaye ameamua kwenda naye ili kuendelea
kuangalia maendeleo yake kama anaweza kuwa fiti siku ya mchezo Jumatano.
Kocha huyo ambaye amekabidhiwa kikosi cha Simba siku chache zilizopita
ameoneshwa kudhamiria ushindi kutokana na ahadi ambayo ameitoa kwa
viongozi na mashabiki wa timu hiyo siku aliposaini mkataba wa
kuifundisha timu hiyo.
Simba itashuka kwenye dimba la Stade du Ville, ambalo linabeba
watazamaji 40,000 na kocha huyo amepanga kuwaanzisha washambuliaji wake
wote wawili Emmanuel Okwi na Nicholaus Gyan baada ya Laudit Mavugo
kubaki Dar es Salaam kutokana na kuwa majeruhi.
Wachezaji waliosafiri na kikosi cha Simba Makipa ni Aishi Salum Manula
na Emanuel Elias Mseja. Mabeki Mohamed Hussein, Erasto Edward Nyoni,
Shomari Kapombe, Ally Shomary, Yusufu Mlipili, Murshid Juuko na Kwasi
Asante.
Viungo ni Mzamiru Yassin, Bukaba Paul, Shiza Kichuya, James Kotei, Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, na Jonas Mkude.
Washambuliaji ni Emmanuel Okwi, Moses Kitandu, Nicholas Gyan na John Raphael Bocco.
Simba inahitaji sare au ushindi ili kusonga mbele raundi ya kwanza ya
michuano hiyo, ambapo huenda ikakutana na Al Maasry ya Misri baada ya
timu hiyo kupata ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Green Buffalo ya Zambia
kwenye mchezo wa kwanza.
Comments