Ufaransa
imekataa ombi la rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize
kusaidia kuwarudisha nyuma waasi wanaotishia kuiangusha serikali yake,
huku Marekani ikiamua kufunga ubalozi wake nchini humo.
Wasiwasi umezidi kutanda nchini humo wakati muungano wa waasi hao
unaojulikana kama Seleka ukizidi kusonga mbele kuelekea mji mkuu Bangui,
kwa madai kuwa serikali imekiuka makubaliano ya amani yaliyosainiwa
mwaka 2007. Lakini rais Francois Hollande wa Ufaransa amekataa ombi la
rais Francois Bozize akisema kuwa muda wa kufanya hivyo ulikwisha.
Marekani yaamua kufunga ubalozi wake
Marekani kwa upande wake imetangaza jana Alhamisi kuwa inasitisha
shughuli zote katika ubalozi wake mjini Bangui, na kwamba balozi wake na
wafanyakazi wengine wa ubalozi huo walikuwa wameondoka nchini humo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Patrick Ventrell,
alisema uamuzi huo ulichukuliwa kwa kuhofia usalama wa wafanyakazi hao,
na kwamba hatua hiyo haihusiani kwa namna yoyote ile na uhusiano wa muda
mrefu wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili. Marekani pia
iliwatahadharisha raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Jamhuri ya Afrika
ya Kati.
Hayo yanajiri wakati viongozi wa kanda hiyo wakijaribu kuratibu
makubaliano ya kusitisha mapigano na waasi walikuwa wamesema
wamesimamisha kwa muda, operesheni kuelekea mji mkuu, ili kuruhusu
mazungumzo kufanyika. Waasi hao wanataka serikali itekeleze makubaliano
ya kuwatawanya na kuwaingiza katika maisha ya kiraia.
"Wapiganaji wanataka pesa walizoahidiwa ili kuweza kujiunga na jamii ya
kiraia, programu ya kuwatawanya ilihusu kuwanyang'anya silaha wapiganaji
lakini yote hayo hayakutekelezwa na ndiyo matatizo makubwa.
Comments