TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
KIPA MUNISHI
AREJESHWA TAIFA STARS
Timu ya Taifa
(Taifa Stars) imeingia kambini jana jioni (Desemba 12 mwaka huu) jijini Dar es
Salaam kujiandaa kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wa Afrika,
Zambia (Chipolopolo) huku Kocha Kim Poulsen akimjumuisha tena katika kikosi
hicho kipa Deogratias Munishi ‘Dida’.
Kocha Poulsen
amemjumuisha tena Munishi kwenye kikosi hicho kuziba nafasi ya Mwadini Ally
ambaye atakuwa nje ya nchi na timu yake ya Azam inayokwenda kushiriki mashindano
maalumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Wachezaji wote
wengine walioitwa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
wamesharipoti kambini hoteli ya Tansoma, na timu imeanza mazoezi leo asubuhi
(Desemba 13 mwaka huu) Uwanja wa Karume, na jioni itafanya mazoezi kwenye uwanja
huo huo.
Kuanzia kesho
jioni (Desemba 14 mwaka huu) itafanya mazoezi Uwanja wa Uwanja wa Taifa wakati
mazoezi ya asubuhi yataendelea kuwa Uwanja wa Karume. Wachezaji ambao bado
hawajaripoti kambini ni Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaocheza mpira wa
kulipwa nchini DRC.
Mechi kati ya
Taifa Stars na mabingwa hao wa Afrika itachezwa Desemba 22 mwaka huu kwenye
Uwanja wa Taifa. Kocha wa Chipolopolo, Herve Renard ameshataja kikosi chake cha
wachezaji 24 kwa ajili ya mechi hiyo.
COASTAL
YAENDELEA KUCHACHAFYA UHAI CUP 2012
Coastal Union
ya Tanga imeendelea kufanya vizuri kwenye michuano ya kuwania Kombe la Uhai
inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi Kuu ya
Vodacom baada ya jana (Desemba 12 mwaka huu) kuifunga Toto Africans mabao
3-1.
Mabao ya
Coastal katika mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Chamazi yalifungwa na
Mohamed Miraji dakika ya 44, Abdul Banda (dk. ya 62) na Ramadhan Shame (dk. ya
83). Toto Africans ndiyo iliyoanza kupata bao dakika ya 30 lililofungwa na
Severin Constantine.
Coastal Union
ilishinda mechi yake ya kwanza mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika
michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji
Uhai.
Nayo Simba
iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya African Lyon katika mechi ya kundi B
iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 12 mwaka huu) Uwanja wa Karume. Miraji Athuman
na Ramadhan Mzee ndiyo walioifungia Simba dakika ya 15 na 47 wakati la African
Lyon lilifungwa dakika ya 57 na Mbela Kashakala.
Polisi
Morogoro iliifunga Azam bao 1-0 kwenye Uwanja wa Karume wakati katika Uwanja wa
Azam, JKT Ruvu iliifunga Tanzania Prisons bao 1-0 lililofungwa dakika ya 16 na
Jacob Mambia. Yanga na Ruvu Shooting zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa
Chamazi.
Katika mechi
iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 13 mwaka huu) Uwanja wa Karume, Oljoro JKT
imeizamisha Kagera Sugar mabao 3-0. Mabao hayo yamefungwa na Hamis Saleh dakika
ya 49 huku Shamir Mohamed akipachika mawili dakika ya 52 na 55.
Michuano hiyo
itaendelea kesho (Desemba 14 mwaka huu) kwa michezo kati ya Mtibwa Sugar vs Toto
Africans (asubuhi- Karume), Coastal Union vs JKT Ruvu (mchana- Karume), Oljoro
JKT vs Yanga (asubuhi- Chamazi), Ruvu Shooting vs Kagera Sugar (mchana-
Chamazi), Mgambo Shooting vs Simba (asubuhi- Chamazi) na African Lyon vs Azam
(jioni- Chamazi).
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Comments