WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamevamia gari lililokuwa
linasafirisha maiti kutoka mjini Morogoro kwenda mkoani Mara kisha
kupora takriban Sh19.8 milioni walizokuwa nazo waombolezaji.
Mhudumu
wa chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya Mkoa Singida, akirekebisha
mapambo ya jeneza lililokiwa na mwili wa marehemu Munchari Lyoba,
mwanafunzi wa SUA , jeneza lililovunjwa na majambazi na maiti kupekuliwa
yakitafuta fedha zaidi baada ya kupora wasindikizaji. Picha na Gasper
Andrew
Katika tukio hilo la kusikitisha lililotokea juzi mkoani Singida,
majambazi hao walivunja vioo vyote vya gari pamoja na jeneza lililokuwa
na mwili wa Munchari Lyoba aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika
Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) cha Morogoro na kumpekua marehemu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya chumba cha kuhifadhi
maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida, mkuu wa msafara uliokuwa
ukisafirisha maiti, Makaranga alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi
saa 7:30 usiku katika gari aina ya Land Cruiser mali ya SUA.
Akisimulia tukio hilo, Makaranga alisema kuwa lilitokea katika Barabara
Kuu ya Dodoma – Mwanza nje kidogo ya Mji wa Singida kwenye kona maarufu
kwa jina la Mohammed Trans kuelekea mkoani Mara.
Alisema kuwa gari hilo pamoja na jeneza, lililobeba viongozi wa
wanafunzi sita na viongozi wengine wanne lilipofika eneo la tukio,
walikuta mawe makubwa yamepangwa barabarani na kuwalazimisha kusimama
ndipo wakavamiwa na kundi kubwa la vijana, ambao walibeba bunduki mbili
aina ya gobore, marungu, mashoka na mawe.
“Walipofika walipiga kioo cha gari letu kwa mbele na kumparaza kwa panga
usoni dereva wetu. Baada ya hapo walivunja vioo vyote na kutuamuru
kutoa kila kitu tulichokuwa nacho,” alisema Makaranga.
Comments