Na Rajab Ramah, Nairobi
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi Nancy Omala anakumbuka kwa uchungu
wakati wezi walipompora kompyuta yake ya mkononi wakati akitoka duka la
kahawa katika Wilaya ya Kati ya Biashara jijini Nairobi.
Wakaazi wa kitongoji cha Eastleigh mjini
Nairobi wakitembea katika wilaya ya biashara. Karibuni Nairobi itakuwa
na kamera za ulinzi ili kuzuwia uhalifu na kusaidia katika uchunguzi wa
polisi. [Na Simon Maina/AFP]
Omala, mwenye umri wa miaka 25, alikuwa ndio kwanza amemaliza kufanya
masawazisho ya mwisho ya kazi yake ya shule na alikuwa karibu
aiwasilishe ili aweze kuhitimu.
"Kwa bahati mbaya, sikuwa na kopi ya akiba ya kazi hiyo", aliiambia
Sabahi. "Wezi walinipora maisha yangu na ilikuwa pigo kwa kazi yangu."
Alisema kuwa wezi wamemfanya asiweze kuhitimu mwezi wa Agosti iliyopita,
kwa hivyo ilibidi aanze tena kazi yake ili aweze kuhitimu mwakani.
"Nyuso zao bado zimo katika akili yangu," alisema. "Nilielezea wasifu
kwa polisi, lakini ni vigumu kuweza kuwapata. Hata kama polisi
wangewapata, bado ni vigumu kuthibitisha kuwa walikuwa wao kwa sababu
hakukuwa na shahidi wengine."
Maafisa wanatumai kuwa hadithi kama ya Omala zitapungua sana kutokana na
kuwekwa kwa kamera za ulinzi 41 katika maeneo yenye uhalifu mwingi
jijini.
"Tulizitambua sehemu za mwanzo kuwekwa kwa kamera kuwa maeneo ya
uhalifu," Waziri wa Mji Mkuu Nairobi Jamleck Kamau aliiambia Sabahi.
"Polisi, wafanya biashara jijini na wananchi walitusaidia kutengeneza
ramani ya maeneo haya."
Mradi huu umetoa kipaumbele kwa maeneo yenye msongamano mkubwa jijini,
Kamau alisema, na maeneo yatakayofungwa kamera hizo ni pamoja na Kituo
cha Mabasi Nchini cha Machakos, Soko la Muthurwa, Soko la Gikomba,
Hospitali ya Taifa ya Kenyatta, Barabara ya Kirinyaga katikati ya mji wa
Nairobi na eneo lote la Wilaya ya Kati ya Biashara.
Comments