KLABU ya El-Merreikh ya Sudan imeamua kufuta mpango wake wa kumsajili mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyesajiliwa na Simba kwa mkopo akitokea Azam.
Uamuzi huo wa El-Merreikh umekuja baada ya mchezaji huyo kutafutwa kwa simu tangu jana, lakini akawa hapatikani.
Mmoja wa viongozi wa El-Merreikh aliyekuwepo Dar es Salaam kufuatilia usajili wa Ngasa, Sheikh Idrisa ameieleza TBC 1 leo asubuhi kuwa, hawamuhitaji tena Ngasa licha ya kukubaliana na klabu za Simba na Azam kuhusu uhamisho wake.
Mbali na kutomuhitaji tena Ngasa, Sheikh Idrisa alisema wamefunga milango kwa wachezaji wote wa Tanzania kwenda kucheza soka ya kulipwa Sudan kutokana na kukerwa na kitendo cha mchezaji huyo.
Uongozi wa El-Merreikh ulikuwa umetoa siku moja kwa Ngasa, kuanzia jana awe amewasiliana nao ili waweze kumwandalia mipango ya safari ya kwenda Sudan kwa ajili ya kupima afya yake na kuangalia mazingira.
Baada ya kuona mchezaji huyo hapatikani hadi leo asubuhi, Sheikh Idrisa alisema wameamua kufuta kabisa mpango wa kumsajili kwa sababu ameonyesha kuwa sio mwanamichezo mwenye kutaka kujiendeleza kimichezo.
Alipotafutwa na TBC 1 leo asubuhi, Ngasa alisema ameamua kubadili namba yake ya simu kwa vile kuanzia sasa hataki kupigiwa simu zaidi ya yeye kuwapigia wale anaowahitaji.
Ngasa alisema pia kuwa, ameamua kufuta mpango wake wa kwenda kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya El-Merreikh kutokana na kutoridhishwa na kiwango cha malipo ya ada ya uhamisho.
Mshambuliaji huyo aliyeng'ara katika michuano ya Kombe la Chalenji, iliyomalizika wiki iliyopita nchini Uganda, alisema anataka kuendelea kuichezea Simba hadi mkataba wake wa mkopo utakapomalizika Mei mwakani.
El-Merreikh imetoa dola 100,000 kwa Simba na Azam kwa ajili ya uhamisho wa mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, ambapo kila klabu itapata dola 50,000.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Ngassa atapokea kiasi cha $75,000 kama gharama ya usajili kwa mkataba wa miaka miwili, na pia atalipwa kiasi cha $ 4,000 kama mshahara kwa kila mwezi.
Kutoweka kwa Ngasa, ambaye pia alikuwa akitafutwa na viongozi wa klabu yake ya Simba bila mafanikio, kumezusha hisia kwamba amefichwa na viongozi wa Yanga, ambayo inataka kumsajili msimu ujao.
Wasiwasi wa Ngasa kufichwa na Yanga ulikuja saa chache baada ya Simba na Azam kufikia makubaliano ya kumuuza mchezaji huyo wa klabu ya El-Merreikh ya Sudan.
Simba na Azam zilifikia makubaliano hayo jana mchana baada ya kikao cha pamoja kati yao na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema jana kuwa, viongozi wa El-Merreikh wamekuwa wakimtafuta Ngasa kwa njia ya simu tangu mchana, lakini hakuwa akipatikana na haieleweki mahali alipokuwa.
Rage alisema wana wasiwasi kuwa, mchezaji huyo huenda amefichwa na wapinzani wao wa jadi Yanga, baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba wanataka kumsajili.
Hata hivyo, Rage alisema Yanga hawana uwezo wa kumsajili Ngasa kwa sasa kwa vile mkataba wake na Simba unatarajiwa kumalizika Mei mwakani. Pia alisema Yanga haina uwezo wa kulipa ada ya uhamisho wake na mshahara wa dola 4,000 kwa mwezi.
Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Bin Kleb alipoulizwa jana, alisema hawezi kusema lolote, isipokuwa atafutwe kuanzia kesho au keshokutwa.
Bin Kleb hakuwa tayari kukubali au kukataa kuhusu klabu yake kumficha Ngasa, zaidi ya kusisitiza kuwa atafutwe katika siku hizo mbili.
Kwa upande wake, Rage aliipongeza Azam kwa uamuzi wake wa kukubali kuketi meza moja na klabu yake kwa ajili ya kufikia uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya mchezaji huyo.Inatoka kwa mdau.
Comments