WAZIRI Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Monduli Mh. Edward Lowassa amewashauri
wabunge wa timu ya Bunge Sports kufikiri juu ya kutunga sera ya michezo
itakayoruhusu kuanzishwa kwa Shule za Michezo (Sports Academy) hapa
nchini.
Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa (wa pili kushoto)
Lowassa ameyasema hayo jana,baada ya kuialika nyumbani kwake timu hiyo
iliyopiga kambi ya jijini Arusha tayari kwa mashindano ya Mabunge ya
Afrika Mashariki jijini Nairobi.
“Nilisikitika kweli Timu ya Taifa ya Kilimanjaro Stars ilipofungwa na
Burundi kwenye mchezo wa pili wa Mashindano ya CECAFA huni Uganda,
pamoja na juhudi za Rais Jakaya Kikwete kuleta makocha bado tumefungwa
na Burundi iliyotoka kwenye vita juzi!.
“Nyinyi ni watunga Sera, ni wachezaji mnajua changamoto zinazofanya
tusifike juu, umefika wakati wa kuwa na Shule za Michezo zinazotambuliwa
na Sera zetu.
“Mpira ni chakula cha Watanzania, wanapenda mpira sana. Napendekeza
baada ya kurejea anzeni kufikiria juu ya kutunga Sera ya kuwa na Shule
za Michezo. Kipingu amejitahidi kuwa na kitu kama hiki lakini amebakia
peke yake hakuna anayemuunga mkono,” alisema Lowassa.
Alisema kuwapo kwa Timu ya Bunge Sports kutasaidia kufikiria juu ya
mafanikio ya mchezo wa mpira wa miguu, pete na michezo mingine.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,Mh.
Amos Makalla aliyeongozana na timu hiyo alimwambia Mh. Lowassa kwamba
serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera za michezo.
Comments