Na Bosire Boniface, Garissa
Picha ya teksi ya pikipiki ya Faith Kabura Makena kwenye barabara za Garissa nchini Kenya inatoa taswira ya nadra sana.
Grace Ruwa Asar, mwanamke wa kwanza kuwa
dereva wa bodaboda Kenya, akimbeba abiria kwenye eneo la Tana River
Delta. [Bosire Boniface/Sabahi]
Makena, mwenye umri wa miaka 30, alisema anajua kwamba kuchagua kwake
biashara hii kumesababisha utata na mara kadhaa huwashangaza wakaazi wa
huko anapowapita.
Teksi za pikipiki, zinazojulikana kama bodaboda nchini Kenya, ni njia
maarufu ya usafiri kwa wasafiri wanaotaka kukwepa foleni kubwa za magari
mijini. Wakati inatoa fursa ya kupata maisha mazuri kwa waendeshaji
wake, hii ni biashara ambayo imekuwa ikitawaliwa na wanaume tu.
Hata hivyo, Makena alisema aliamua kuipa changamoto imani iliyopo na
kuwa dereva wa bodaboda kwa sababu ni chanzo kizuri cha mapato ya
kumuhudumia mtoto wake wa kiume wa miaka 6 na wazazi wake, ambao ana
jukumu la kuwatunza kifedha.
"Mwanzoni nilikuwa ninakerwa na namna watu walivyonichukulia lakini
kutokana na uungaji mkono wa familia yangu na marafiki, nilisonga
mbele," aliiambia Sabahi. "Wiki za mwanzo zilikuwa ngumu kwa sababu
sikuweza kupata wateja. Mteja mmoja hata aliwahi kuniambia kwamba
nilikuwa ninatania na asingeliweza kuamini usalama wake barabarani
kwenye mikono ya dereva mwanamke."
Faith Kabura Makena alivunja kikwazo cha kijinsia kwa madereva wa kike wa bodaboda mjini Garissa. [Bosire Boniface/Sabahi]
Makena alisema kwamba binamu yake alimfundisha kuendesha pikipiki kwa
nia ya kujifurahisha tu. "Kutokana na uchache wa ajira, ilinipitikia
kwamba kile nilichojifunza kwa kujifurahisha kinaweza kuwa fursa za
kuzalisha kipato," alisema.
Makena, ambaye mwanzoni alikuwa akimiliki duka, amekuwa dereva tangu
mwezi Januari, akiwa kwa wastani anapata shilingi 20,000 (dola 233) kwa
mwezi. Kwa sasa anafanya kazi na dereva mwingine lakini anatarajia
kuweka akiba hadi shilingi 80,000 (dola 931) kufikia mwezi Februari ili
aweze kununua pikipiki yake mwenyewe na kuwa dereva anayejitegemea.
Lengo lake kuu, hata hivyo, ni kuwa mwalimu wa sekondari ya juu. Makena
alisema amekuwa akiweka fedha kila mwezi kulipia shule, ambako ataanza
mwezi Juni ujao.
Comments