UONGOZI wa klabu ya Mtibwa Sugar umeiwekea ngumu klabu ya Yanga kuhusiana na ombi la kurudishwa kipa wake, Shaaban Kado kwenye timu hiyo au kusajiliwa na timu ya Coastal Union.
Mratibu wa timu hiyo, Jamal Bayser alisema kuwa walipokea barua kutoka Yanga ikiwataka kumrejesha kipa wao huyo kwa vile amesajili kwa mkopo na wao kuweka ngumu kutokana na makubaliano yao kuhusiana na kipa huyo.
Bayser alisema kuwa wao walikubaliana na Yanga kumchukua Kado kwa msimu mmoja, na kushangazwa na hatua ya klabu hiyo ambayo ilibadili msimamo wake hasa baada ya kipa wao, Yaw Berko kutolewa kwa mkopo.
Alisema kuwa Yanga pia iliwataarifu kuhusiana na mpango wao wa kutaka kumpeleka Kado Coastal Union, lakini ikashindikana tena kwa kipengele kile kile cha mktaba wa awali.
“Kado atacheza Mtibwa Sugar mpaka mwisho wa msimu kama ilivyokuwa makubaliano yetu, hivyo hawezi kurejeaYanga wala kwenda Coastal Union,” alisema Bayser ambaye ameongeza nguvu timu yake kwa kumsajili mchezaji wa zamani wa Vital’O ya Burundi, Stanley Minzi na kumpandisha kinda wao, Rajab Zahir.
Alisema kuwa hata suala la Rashid Gumbo kuichezea timu hiyo kwa mkopo lilikuwa na utata na kuwaachia Yanga kumalizana kwanza na Gumbo. Alifafanua kuwa pamoja na vyombo vya habari kutangaza kuwa Gumbo yupo Mtibwa, ameamua kuweka wazi kuwa hawaja mpokea kiungo huyo.
Vile vile, African Lyon imekubali kuwapokea wachezaji watatu kutoka Yanga kwa ajili ya kuhimarisha kikosi chao. Wachezaji hao ni Ibrahim Job, Salum Telela na Idrisa Senga.
Katibu mkuu wa Africa Lyon, Brown Ernest alisema kuwa wamekubaliana na Yanga kuhusiana na kuwachukua wachezaji hao kwa mkopo na vile vile kuongeza wachezaji wengine, Yusuph Mgwao na Valentine Njaka, Mcameroon aliyekuwa anaichezea JKT Oljoro.
Wakati huo huo; Mabingwa wa soka wa Afrika Mashariki na Kati , Yanga wanatarajiwa kuondoka nchini, Desemba 28 kwenda Uturuki, kocha mkuu , Ernie Brandts amesema kuwa anashindwa kutangaza majina ya wachezaji kwa ajili ya safari hiyo imetokana na usiri mkubwa wa zoezi la usajili lililomalizika juzi saa 6.00 usiku.
Brandts amesema kuwa imemuwia vigumu sana kutangaza kikosi cha wachezaji kwani mikoba yote kuhusiana na usajili hasa wachezaji wanaotolewa kwa mkono anayo mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na mashandano, Abdallah Bin Kleb.
Alisema kuwa mpaka sasa hakuwa anajua ni mchezaji gani atatolewa kwa mkopo zaidi ya usajili wa pacha wa Mbuyu Twite, Kabanga Twite, ambaye imetokana na mapendekezo yake ya kuhimarisha safu ya ushambuliaji wa timu hiyo.
“Ni vigumu kujua nani amesajiliwa kwa sasa, hii inatokana na ukweli kuwa suala lote anafanya Abdallah, mimi najua usajili wa Kabanga tu, nani anatolewa kwa mkopo sijui mpaka sasa,” alisema Brandts.Inatoka kwa mdau.
Comments