Na Bosire Boniface, Garissa
Jamii ya Kisomali nchini Kenya imelaumiwa sana kwa mashambulizi ya
al-Shabaab, lakini wachambuzi wa masuala ya usalama wanaonya kwamba
kuwasingizia Wasomali kunaongeza hatari ya mashambulizi ya baadaye kwani
wanamgambo wa jamii nyingine wanaweza kufanya shughuli zao za kigaidi
bila kufahamika.
Raia wa Uswisi Magd Najjar (kulia)
akifikishwa mahakamani mjini Nairobi kushitakiwa rasmi kwa kuwa na
mafungamano na al-Shabaab. Najjar ni mmoja wa washukiwa wengi wa
al-Shabaab wenye utaifa wa nchi mbalimbali wanaodhaniwa wapo Kenya.
[Simon Maina/AFP]
Aden Duale, mbunge wa jimbo la Dujis, alisema Wakenya kwanza huwashuku
watu kutoka jamii ya Kisomali popote panapofanywa mashambulizi nchini
Kenya.
"Mashambulizi hayo kawaida huleta dhana potofu na kuyahusisha na jamii
ya Kisomali, ingawa hakuna mtu aliyeandikwa usoni pake kwamba ni
mwanachama (wa kundi la kigaidi). Kuwailenga jamii ya Kisomali ni
kutafuta majina na chuki dhidi ya wageni," aliiambia Sabahi.
Katika miezi ya hivi karibuni, vikosi vya usalama vya Kenya vimejibu
mashambulizi ya kigaidi kwa kuwasakama wakimbizi, ikiwemo kuwakamata kwa
wingi watu wa jamii ya Kisomali. Wiki iliyopita, serikali ya Kenya
ilitangaza kwamba wakimbizi nchini humo lazima warudi kwenye kambi,
kwani usajili na huduma zitasitishwa mijini.
Siku ya Alhamisi (tarehe 20 Disemba), Shirika la Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa liliitaka Kenya kujiepusha kuwalaumu wakimbizi kwa vitendo vya
vurugu nchini humo.
Wakenya wana jukumu kubwa kwenye ugaidi
"Uwanachama wa al-Shabaab umevuka mipaka ya jamii ya Kisomali," alisema
Meja Mstaafu wa Jeshi la Kenya Bashir Haji Abdullahi, ambaye anafanya
kazi ya ushauri wa masuala ya usalama.
Comments