Rais
wa Marekani Barack Obama ameahidi kutumia mamlaka yake yote kuhakikisha
kuwa mikasa ya mauwaji yanayotokana na mashambulizi ya kiholela ya
risasi haitokei tena.
Akizungumza katika mkesha wa maombolezii mjini Newtown ya watu 26
waliouawa katika shule moja ya msingi wakiwemo watoto 20, Obama amesema
Marekani haifanyi vya kutosha katika kuwalinda watoto wake, na akaahidi
kwamba katika wiki zijazo, ataanzisha juhudi za kupunguza mashambulizi
kama hayo nchini humo.
Lazima kufanywe mabadiliko
Rais Obama amesema matukio ya mauwaji ya mashambulizi ya risasi hayawezi
tena kuvumiliwa na ni lazima yafikie kikomo. Na kwa kutimiliza hilo, ni
lazima pawepo mabadiliko. Rais huyo wa Marekani ameeleza mapenzi yake
na maombi ya taifa kwa jumla kwa familia za wahanga wa mauwaji hayo,
akisema Wamarekani wote wanasimama pamoja nao katika kuomboleza vifo
hivi vya kikatili.
Rais Obama ametoa wito wa dharura kwa Wamarekani kufanya kila wawezalo
kuzuia kutokea tena mikasa isiyo na idadi ya ufyatuwaji risasi ambayo
imeitia hofu nchi hiyo. Tangu kuchaguliwa kuwa rais, Obama ameshuhudia
matukio manne makuu ya mauwaji ya kiholela kupitia risasi, lakini
kumekuwa na visa vingine vidogo vilivyotokea katikati ya matukio hayo.
Hakuna sheria inayoweza kuangamiza maovu duniani
Obama amekiri kwamba hakuna sheria yoyote inayoweza kutokomeza uovu
duniani au kuzuia kila aina ya mauwaji katika jamii, lakini akadokeza
kwamba atatafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Comments