MAASKOFU nchini, jana walitumia ibada za Krismasi kukemea maovu, huku
baadhi yao wakiwatuhumu matajiri nchini kuwa ndiyo kiini cha vurugu
zilizosababisha kuchomwa kwa makanisa yao hivi karibuni.Wakihubiri kwa
nyakati na makanisa tofauti, viongozi hao walisema uhasama huo dhidi ya
Wakristo ulioanza kujengeka katika siku za hivi karibuni, unafadhiliwa
na baadhi ya matajiri kwa masilahi yao binafsi.
Katika
tamko lao lililotolewa na Umoja na Makanisa Tanzania, maaskofu hao
wameitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya mbegu za chuki
zinazopandikizwa ili kuwafarakanisha Watanzania kwa misingi ya imani za
dini.Tamko hilo ambalo litarejewa Desemba 30, mwaka huu, ni makubaliano
ya pamoja kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Moravian, Anglikana, Pentekoste, Wasabato na Kanisa Katoliki.
Askofu Dk Martin Shao wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini akisoma tamko hilo
wakati wa ibada ya pamoja, alidai kuwa baadhi ya vyombo vya habari vya
kidini, vinawachochea watu ili wawaue maaskofu na wachungaji mbalimbali
wa makanisa.
Pia, alihoji kauli zinazoenezwa kuwa nchi hivi sasa inaongozwa kwa mfumo
wa Kikristo ilihali asilimia 90 ya viongozi wa juu nchini ni
Waislamu.“Labda niwakumbushe, viongozi wote waandamizi wa ngazi za juu
nchini, asilimia 90 ni Waislamu, itakuwaje nchi iendeshwe kwa mfumo wa
Kikristo?” alihoji Askofu Shao.
Aliwataja kuwa ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa
Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).“Kule
Zanzibar, asilimia 100 ya viongozi wote ni Waislamu na si kweli kwamba
Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa ya kuongoza,” alisema na kuongeza:
“Hata uwakilishi kwenye Tume kama ya kuandikwa kwa Katiba Mpya, theluthi
mbili ya wajumbe wake ni Waislamu… Nchi hii haina mfumo wa Kikristo,
bali ni nchi yenye mfumo wa kidemokrasia.”Aliitaka Serikali ithibitishe
ukweli kuwa haiendeshwi kwa mfumo wa Kikristo badala ya kukaa kimya
wakati maneno hayo ya uchochezi yanaenezwa hadharani.
Comments