WAKATI
wakongwe wa siasa wakimhadharisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa,
kutofuata mashabiki wanaomtaka ahame CCM ambako amelelewa na ndiko
anakoheshimika, madiwani 20 wa chama hicho katika Jimbo la Monduli,
wamejiunga na Chadema.
Madiwani
hao wameingia Chadema na kufuatwa na wenyeviti sita wa vijiji pamoja na
viongozi wa jumuiya za CCM, huku wakimwomba Lowassa ambaye ni Mbunge wa
jimbo hilo, kufanya kinachoitwa ni uamuzi mgumu wa kuwafuata, baada ya
CCM kukata jina lake sambamba na wagombea urais wengine 33, wakiwemo
waliowahi kuwa mawaziri wakuu kama yeye.
Akizungumza
jana katika mkutano wa hadhara, kabla ya kukabidhi kadi yake na za
wenzake 19 wa CCM kwa viongozi wa Chadema, kiongozi wa Madiwani hao,
Julius Kalanga kutoka Kata ya Lepurko, alisema wamefanya uamuzi aliouita
mgumu, ambao Lowassa amekuwa akiuzungumza.
“Sisi
tumeamua kujiunga Chadema kutafuta haki na kuondoka CCM ambako
wanachakachua Katiba ya Chama kwa kumpitisha kiongozi wanayemtaka,
badala ya kufuata Katiba na wananchi wanachotaka. “Tunamwomba Mheshimiwa
wetu Lowassa, atufuate huku Chadema, afanye uamuzi mgumu aliokuwa
akisema kila siku na asiogope kuhama... atakuwa amefanya uamuzi wenye
tija kwa Taifa,” alisema Kalanga.
Diwani
huyo pia aliwasihi wananchi kufuata madiwani wao wanakokwenda kwa sababu
hata huko watachukua fomu na kugombea ili kuing’oa CCM madarakani.
Waliohama
Madiwani
waliohama chama ni wa kata ya Engaruka, Engutoto, Esilalei, Loksale,
Majengo, Makuyuni, Meserani, Nalalani, Lemooti, Moita, Monduli Juu,
Monduli Mjini, Mferejini, Mswakini, Mto wa Mbu, Migungani, Selela,
Sepeko na Lashaini.
Madiwani
na viongozi hao ni Kalanga mwenyewe, Edward Lenanu, Bazir Siamini, Sigur
Olekibinti, Loti Yamat, Goodluck Lerunya, Pashet Sengurumi, Yase Runja,
Gidion Kimongishu, Dora Kipuyo, Mary Morindat, Sara Lomayan na Halima
Lusinde.
Wengine
ni Dotto Mlacha, Hawa Nyambiry, Alex Kamanda, Sion Kapela, Maria Lemta,
Onesmo Naikoyo, Shaban Adam, Enditosidai Naikulo na Elifuraha Simon.
Pia yupo
Dinna Solomon, Loti Naparana, Jocy Laizer, Edward Mathayo, Piniel
Loning’o, Napir Mukare, Inot Leringa, Kalaine Lowassa, Maria Mepukori,
Mary Stivin na Edward Kone.
Ushauri wa wakongwe
Mwito huo
wa madiwani wa Monduli, unatofautiana na ushauri wa kada mkongwe wa
CCM, Steven Mashishanga, aliyekaririwa akimtaka Lowassa atulie na
aachane na ushawishi wa watu wanaomtaka ahame chama hicho.
Mashishanga
katika mahojiano yake na gazeti moja la kila siku juzi, alimkumbusha
Lowassa kuwa bado ni kiongozi anayeheshimiwa na jamii na kumuasa kuwa
kama anahisi ameonewa, asamehe.
Akifafanua
hoja zake, Mashishanga alisema wanaomshawishi Lowassa ahame CCM na wale
wanaohama chama hicho kwa sababu ya kukatwa kwa jina la Lowassa katika
kuwania urais, si wana CCM wa uhakika.
Kwa
mujibu wa Mashishanga, ndani ya CCM mgombea akiteuliwa, wanachama
huachana na yaliyopita na kuwa wamoja kwa ajili ya kukiendeleza chama.
Malaigwanani
Mbali na
Mashishanga, pia wazee wa kimila wa jamii ya wafugaji wa Kimasai,
maarufu malaigwanani kutoka Wilaya ya Monduli, nao wamemuomba Lowassa
kuendelea kuwa kada wa CCM, kwa sababu ndicho chama kilichomlea na
anakijua.
Mmoja wa
malaigwanani, Mzee Joseph Mesopiro, kutoka Kata ya Sepeko, alikaririwa
na vyombo vya habari kwa niaba ya malaigwanani akisema, wanakusudia
kutuma ujumbe maalumu kwa Lowassa, utakaomshauri asihame CCM kama baadhi
ya watu aliowaita wapambe wanavyomshauri.
Laigwanani
mwingine, Julius Laizer kutoka Kata ya Moita, alisema bado anaamini
kuwa CCM itaendelea kubaki imara, hata kama baadhi ya watu watakihama.
Lazier
alisema viongozi waliolelewa na kukuzwa CCM, wanaamini chama hicho
kitaendelea kuwa imara na hawako tayari kukubali ushawishi wowote wa
kutaka wahamie upinzani.
Naye
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Lepurko wilayani Monduli, Njoput Alami,
alikaririwa akibeza taarifa za kushawishi watu kuhama CCM kwa kisingizio
cha Lowassa kukatwa katika majina ya wawania urais, akiziita ni kelele
za wapambe wanaohofia kukosa fursa walizotarajia, iwapo Lowassa
angeteuliwa kuwa mgombea urais wa CCM.
Mwenyekiti
wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa aliwakaribisha na kusema
Chadema watu wote wanapendana na hakuna ukubwa wala uongozi, hivyo
wanapokuja huko ni kazi moja ya ukamanda kuwatumikia wananchi.Chanzo ni http://www.mjengwablog.com
Comments