=========
JESHI la Polisi Visiwani Zanzibar, limekiri kutokea kwa tukio la kushambuliwa kwa risasi watu wawili, mapema leo asubuhi katika Mkoa wa Kusini Unguja na kukanusha vikali kuwa tukio hilo halijatokea kwenye vituo vya kujiandikisha katika daftari la wapiga kura.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kusini Ugunja, Juma Khamis, akizungumza na FikraPevu.com amesema watu wawili tu ndio waliopigwa risasi na kundi la watu ambao hawajafahamika mara moja na kuwa sio ndani ya vituo au karibu na vituo vya kujiandikishaia wapiga kura.
Amewataja watu waliojeruhiwa vibaya katika tukio hilo kuwa ni pamoja Hery Makame (49), na Ramadhani Hija, wakazi wa Mkoa wa Kusini Magharibi ambapo taarifa za awali zilieleza kuwa watu hao walipigwa risasi katika eneo la Nganani Makunduchi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa watu hao walikuwa nje ya Vituo vya kuandikishia kura. Uchunguzi wa awali wa Polisi umebaini kwamba watu waliojeruhiwa kwa risasi walikuwa wanajaribu kuwazuia watu waliotuhumiwa kujiandikisha bila kutimiza vigezo (Hawakuwa wenyeji wa eneo hilo) na ndipo zilipotokea vurugu hizo.
Majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar, na hali zao zimeelezwa kuwa sio za kuridhisha kwani hali za afya zao imepelekea hata Polisi kushindwa kuwahoji ili kuchukuliwa maelezo yao.
Mapema leo Julai 4, 2015 Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, amelitaka Jeshi la Polisi kufuatilia kwa kina tukio hilo, kutokana na kwamba linaweza kusababisha wananchi kususia zoezi la uandikishaji wapiga kura.
“Polisi ni suala la Muungano, tuna Jeshi la Polisi moja na kazi yao ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Tunalitaka Jeshi hili lihakikishe wale wote waliofeatua risasi na kujeruhi watu wamekamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria” alieleza Prof. Lipumba.
Katika mitandao mbalimbali ya kijamii nchini (Sio FikraPevu.com), imeripotiwa kuwa watu waliopigwa risasi na watu waliofunika nyuso zao ni wanachama wawili wa CUF na kwamba tukio hilo limetokea kwenye kituo cha kuandikishia wapiga kura cha Makunduchi.Inatoka http://www.jamiiforums.com
Comments