Kocha wa klabu ya ‘Wekundu wa Msimbazi’ Simba amesema anataka kuongezwa
kwa golikipa mwingine kwasababu Ivo pekeyake ameonekana hatoshi huku kocha huyo
akiongeza kwamba, magolikipa wengine wa kikosi hicho bado hawajaiva kuwa tayari
kuhimili mchakamchaka wa ligi kuu.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba Hans Poppe amethibitisha kuwa
timu yao inahitaji golikipa mwingine na huenda watatumia mashindano ya Kagame
ili kupata kipa atakae jiunga na klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa
Msimbazi.
“Sisi bado tunaendelea, bado tunahitaji golikipa kutokana na maagizo ya
kocha, Ivo pekeyake hatoshi kama akiumia tutapata shida na hawa wengine
hawajaiva sawasawa kuwa wachezaji wakuaminika kwenye kikosi cha kwanza, kwahiyo
wanahitaji muda wa kuendelea na mazoezi na mafunzo kadha wa kadha”, amesema
Hans Poppe.
“Timu inatakiwa kuwa na kipa ambaye yuko tayari kama alivyo Ivo, maana
kuna kuugua, kuna kuumia na kuna kadi tatu za njano na kadi nyekundu. Sasa yote
haya au mojawapo linaweza likamsibu kipa tuliyenae halafu tukashindwa kuwa na
mbadala”, ameongeza.
“Kuhusu kipa, tunaangalia sehemu nyingi. Kuna Kagame Cup inakuja hapa
tutaangalia tunaweza tukaibuka na kipa hapahapa”, alimaliza.
Golikipa anaechipukia kutoka ndani ya klabu hiyo Manyika Jr, ameshindwa
kuaminiwa baada ya kudaiwa kiwango chake kushuka tofauti na alivyoanza ambapo
baadhi ya wadau wa soka walianza kumtabiria makubwa kwenye klabu hiyo.Inatoka kwa mdau
Comments