"Masikio hayawezi kuvuka kichwa, kiongozi wa serikali usiyetaka kuambiwa ukweli na chama nenda kalale, acha kazi." Hii ni kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Nape Nnauye aliyoitoa wakati akikemea ule aliouita uzembe wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Nape na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana bado wanaendelea kupaza sauti kuwa baadhi ya wateule wa mwenyekiti wao wa chama, Jakaya Kikwete hawaendani na kasi ya kutumikia jamii.Mwaka jana waliibuka na kibwagizo kuwa, serikali yao inayoongozwa na Rais Kikwete ina rundo la mawaziri mizigo, utashi wao ukawa ni kumtaka mwenyekiti awatimue wasikigharimu chama.
Wakati kionjo hicho cha mawaziri mizigo kikionekana kupoa, wameibua kingine kinachoitwa waziri mzururaji; wakimaanisha Nyalandu. Wametoa hoja ang'olewe akalale kwa kuwa ameonesha kuishindwa nafasi ya uwaziri.
Wamesema
wazi kuwa, masikio hayazidi kichwa, tafsiri ni kwamba wanaoingoza
serikali ni masikio ya CCM ambacho ndiyo kichwa cha rais hadi katibu
tawala. Hapa ndipo ninapoitafakari CCM na serikali yake kiasi cha
kuchanganyikiwa.
Kwa nini?
Nape na Kinana wanaposema karibu kila walikopita wamekutana na migogoro
ya ardhi ikiwahusisha wananchi, hifadhi za taifa na kwa upande mwingine
wawekezaji na waziri yupoyupo tu; anazurura, kuna kitu cha kutafakari.
Najiuliza;
Kinana anapomuona mzururaji Rais Kikwete aliyemchagua katika nafasi
hiyo ya uwaziri anakuwa wapi, kalala? Nape anapomuona Nyalandu kuwa
ameshindwa kutekeleza jukumu lake; Rais Kikwete, kasafiri?
Nachanganyikiwa kabisa!
Ukifuatilia
ziara za Nape na Kinana zinazoitwa za kujenga chama kila walipopita
viongozi hao hotuba zao nyingi zimejaa ukosoaji kwa baadhi ya watendaji
wa serikali, kwa vinywa vyao wamekiri hadharani kuwa udhaifu huo
unakidhoofisha chama chao.
Jambo la
kujiuliza; hivi kichwa (CCM) na masikio (watendaji) havina ushirikiano
ndiyo maana jamii inashuhudia mkanganyiko huo wa kimtazamo? Ikiwa viungo
hivi havishirikiani katika utendaji, wananchi wanavigawanyaje ili
kinachoonekana dhaifu wakichukie?
Tangu
lini mchongoma ukazaa machungwa? Kamwe chemchemi ya maji haiwezi kutoa
maji matamu na maji machungu. Naomba nisikilizwe hoja zangu kwa
makini.CCM ya Nape na Kinana, mwenyekiti wake ni Rais Kikwete ambaye ni
mkuu wa uteuzi wa karibu nafasi zote nyeti za nchi hii, nafasi hizohizo
ndizo zinazopigiwa kelele na wasafisha chama kuwa ni dhaifu ki-utendaji!
Kwa nini
tusifike mbali zaidi ya fikra hizo, tuvuke mipaka ya ufahamu mpaka
tuusogelee ukweli kuwa anayewaangusha siyo Nyalandu na uzururaji wake
bali aliyemteua ambaye ni mwenyekiti wa CCM.
Nashangaa kuaminishwa kuwa chama kinaweza kuwa mtetezi wa wanyonge kwa kiwango wanachoonesha akina Kinana, kuipita serikali ambayo inaongozwa na mwenyekiti wa Kinana.
Nashangaa kuaminishwa kuwa chama kinaweza kuwa mtetezi wa wanyonge kwa kiwango wanachoonesha akina Kinana, kuipita serikali ambayo inaongozwa na mwenyekiti wa Kinana.
Hivi
mashauriano ya chama kifanye nini hawa akina Nape wanayafanyia nyumbani
kwao au ofisini? Wanajipangia watakavyo au vikao vya chama na ridhaa ya
viongozi wa ngazi za juu akiwemo mwenyeti ndiyo vinavyotoa baraka ya
ziara na kupokea mrejesho wa kilichofanywa na watumwaji!
Ikiwa
chama kinaongozwa kwa mfumo, iweje rais ambaye ni mwenyekiti asijue
kuwa, Nyalandu ni mzururaji na kumtimua kazi mara moja! Waliitwa
mawaziri mizigo wakaendelea kudunda kwenye nafasi zao; Nyalandu kaambiwa
aache kazi lakini bado anapanda ndege na kulipwa mshahara unaotokana na
kodi za wananchi.
Naomba
Nape awaambie wananchi wafanye nini ili watenganishe kichwa na masikio
kwa sababu wamechoshwa na umaskini. Asipofanya hivyo ipo siku wataamua
kukata shingo, wakiondoe kichwa pamoja na masikio yake kisha wavitupe
jalalani! Nachochea tu.CHANZO: GLOBAL PUBLISHER
Comments