Baraza la
Sanaa la Taifa (BASATA) lenye dhamana ya kufufua, kukuza na kuendeleza
Sanaa kwa kushirikiana na taasisi ya Ako'mungoma Poverty Alleviation
Organization (APAO) linaendesha programu ya wiki tatu ya Sanaa kwa
watoto katika Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa Sera ya Taifa ya Utamaduni ya mwaka 1997 sura ya 9.6.16 Baraza
linaelekezwa kushirikiana na wadau katika kuendesha matukio mbalimbali
ya sanaa kama programu hii ya watoto.
Programu
hii ya Sanaa kwa watoto ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 07/03/2015
na kuhusisha maonesho, inatarajia kushirikisha watoto 215 ambapo 100
wanaishi katika mazingira magumu eneo la Mbutu - Kigamboni na wengine
100 kutoka shule za Msingi Gomvu na Mbutu. Aidha, watakuwepo wanafunzi
waalikwa 15 kutoka shule ya msingi Msimbazi iliyopo wilaya ya Ilala.(P.T)
Programu
hii ambayo mwaka huu inadhaminiwa na Kampuni ya Mohamed Enterprises na
Haakneel production (T) Ltd inalenga kukuza vipaji vya watoto katika
fani za uchoraji, maigizo hususan majigambo na ngoma za asili. Pia
tunatarajia udhamini toka wadau na makampuni mengine.
Kilele
cha programu hii yenye kauli mbiu ya "Amani na Uchaguzi 2015"kitapambwa
na burudani ikiwemo mpira wa miguu kutoka kwa watoto wa Kituo cha APAO
na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kutoka jimbo la Kigamboni Mheshimiwa Faustine Ndugulile.
Aidha
programu hii ni mwendelezo wa programu ya Sanaa kwa watoto ya Baraza
iliyoanza tangu miaka ya 80 ambayo ilipata kuibua na kukuza vipaji vya
wasanii kama Mrisho Mpoto na Masoud Kipanya ambao hadi sasa wanafanya
vizuri.
Kwa mwaka
2014 programu hii iliendeshwa katika wilaya ya Ilala kwa kushirikisha
shule tano (5) ikiwemo ya Buguruni Viziwi na ilidhaminiwa na kampuni ya
Msama Promotion.
Baraza
linachukua fursa hii kuwaalika wananchi na wadau wote wa sanaa kufika
kwa wingi kushuhudia vipaji vya sanaa walivyonavyo watoto.
Comments