Kaimu Kiongozi wa serikali shughuli za bunge pia ambaye ni Waziri wa Uchukuzi ,Samuel Sitta, akiagana na aliyekuwa mbunge wa Kioma Kaskazini ,Zitto Kabwe.
Ikiwa ni siku moja tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kutangaza kung'atuka katika nafasi yake ya ubunge, Bunge limeeleza kuwa mbunge huyo atapata mafao yake yote kama wabunge wengine.
Zitto ambaye alitangaza juzi bungeni kuwa anaondoka baada ya kuvuliwa unanachama wa Chadema aliahidi kuwa 'Mungu akipenda' atakuwa tena ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria Novemba mwaka huu baada ya uchaguzi mkuu.
Kuondoka kwa mbunge huyo pia kunaifanya nafasi ya uenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali(PAC) kuwa wazi kwa kuwa ndiye aliyekuwa akiishikilia hadi alipotangaza rasmi juzi kuachia ubunge.
Akizungumzia uamuzi wa Zitto na juu ya mafao yake baada ya kuamua kuondoka mwenyewe, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kuwa mbunge huyo atalipwa mafao yake yote.
"Unajua
Chadema wametangaza kumvua uanachama Zitto lakini hawajampa barua, sasa
yeye ameona kuwa kuliko kuendelea na ubunge wake ni vyema akakaa kando.
Kutokana na suala hilo atalipwa tu mafao yake yote,"alisema Joel.
Katika
hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa PAC wamesikitishwa na kuondoka kwa
Zitto kabla ya muda wa Bunge la 10 kumalizika huku wakimwelezea ni
kiongozi aliyeweza kuwaunganisha katika kamati bila kujali itikadi za
vyama.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, wajumbe hao walisema aliwafanya wajumbe wa
kamati hiyo kuwa familia na aliwaamini na kuwaheshimu wote.
"Ni mtu aliyekuwa na ushirikiano na aliweza kutuunganisha bila kujali itikadi.
Alitufanya
kama familia na alituamini na kutuheshimu. Tunamtakia kila la kheri
katika mipango yake ijayo,"alisema Ismail Aden Rage (Tabora Mjini).
Mbunge wa
Mkwamtipura, Kheir Ali Khamis alisema kujiuzulu kwa Zitto ni suala la
Kikatiba asingeweza kuendelea kushika nafasi hiyo.
"Hili ni suala la Kikatiba haki ya kuwa mbunge inaondolewa ukishakuwa si mwanachama wa chama cha siasa,"alisema.
Alisema kutojiondoa mwenyewe kungeleta mgogoro kati yake na chama chake kwa kuwa tayari walishamvua uanachama.
Comments