Fred Felix Minziro
Yanga
inaumana na JKT Ruvu ya Fred Felix Minziro leo kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam, lakini ni kocha mkuu wa kikosi hicho cha wanajeshi
anayeweza kutibua hesabu za mwenzake wa Yanga, Hans Pluijm kusaka
ubingwa.
Minziro
aliyekulia na kucheza soka Yanga kwa maisha yake yote ya miaka 13,
aliinoa timu hiyo kabla ya kutimuliwa, anakutana nayo (Yanga) ikiongoza
ligi ikiwa na pointi 37 na kufuatiwa na Azam yenye pointi 36 na Simba ni
ya tatu ikiwa na pointi 32.
Kocha huyo alisema Yanga wasitarajie mteremko kwao na watakomaa nao leo kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu.
"Tuko
vizuri na Yanga wasitarajie mteremko kwetu, tutacheza kwa kiwango
kikubwa kuhakikisha tunaibuka washindi, najua ni timu nzuri na inaongoza
ligi lakini hata sisi tuko pabaya tunahitaji kujinasua na kupanda
nafasi za juu ili kukwepa kushuka daraja," alisema Minziro.
Kwa upande wake, Pluijm amekiri kuwa hautakuwa mchezo rahisi kuikabili JKT Ruvu ambayo ni timu ngumu kama ilivyo ligi yenyewe.
Timu hiyo
hivi inaikabili JKT Ruvu ikiwa na presha kwani inahitaji ushindi kwa
hali yoyote ile kutokana na wapinzani wao, Azam kuwafuatia kwa karibu.
Pluijm
aliliambia gazeti hili kuwa wamejiandaa vizuri, ingawa haitakuwa kazi
rahisi kwao kupata ushindi mbele ya wanajeshi hao kwani ligi ni ngumu
hivi sasa na kila timu iko katika kiwango kizuri.
Alisema amewaelekeza wachezaji wake kuichukulia kwa umakini mkubwa michezo yote iliyobaki ili waweze kushinda na kutwaa ubingwa.
"Ligi ni
ngumu na kila timu imeonyesha uwezo mkubwa na ndiyo maana nasema
haitakuwa kazi rahisi kushinda dhidi ya JKT Ruvu, lakini tumejiandaa,
wachezaji wangu wako katika kiwango kizuri na naamini tutapata pointi
zote tatu.
"Kikubwa
ni kushinda kila mechi iliyo mbele yetu, hatuhitaji kupoteza chochote
maana mpinzani wetu Azam anatufuatia kwa kasi hivyo lazima tupambane
kuhakikisha kila mechi inakuwa kama fainali kwetu, nawaamini wachezaji
wangu watafanya kazi nzuri na kuweza kupata ushindi kesho (leo),"
alisema Pluijm.
Hata
hivyo, Yanga itamkosa mshambuliaji wake mahiri, Amissi Tambwe mwenye
kadi tatu za njano, kiungo Andrey Coutinho aliye majeruhi pamoja na
Jerryson Tegete anayesumbuliwa na maumivu ya bega.
Mrisho
Ngassa aliyekuwa na maumivu ya nyama za paja na kuukosa mchezo uliopita
dhidi ya Mgambo Shooting amerejea kikosini na kufanya mazoezi na wenzake
jana asubuhi, ingawa daktari wa timu hiyo Juma Sufiani alisema
watamwangalia atakavyoamka leo ili kujua maendeleo yake na kama atacheza
mchezo wa leo au la.
Hata
hivyo, pia kiungo Said Juma Makapu aliyezimia uwanjani dakika za mwisho
katika mchezo dhidi ya Mgambo amerejea na kufanya mazoezi na wenzake
jana asubuhi.
JKT Ruvu itamkosa Zubery Napho ambaye alipata maumivu katika mazoezi wakati ikijiandaa kuikabili Ndanda wiki iliyopita.
Chanzo:Mwananchi
Comments