Mkutano Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) ambao hukutanisha
viongozi wa Klabu za Ligi Kuu ya Soka Bara na Ligi Daraja la Kwanza,
uliofanyika Februari 28 mwaka huu, umejadili mambo mbalimbali ikiwa ni
pamoja kujulishwa taarifa za kupatikana kwa mdhamini wa Ligi Daraja la
Kwanza msimu ujao, ambaye ni Azam Media.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Mtendaji wa Bodi hiyo, Fatma
Shibo, alisema kuwa katika mkutano huo pia wajumbe walijadili utendaji
wa kazi za kila siku za bodi hiyo na mfumo wa tiketi za kieletroniki
ambazo zinatumika.
Shibo alisema kuwa wajumbe wa bodi hiyo pia walizungumzia matukio ya
vurugu zinazotokea kwenye viwanja ambavyo ligi hizo huchezwa na kuahidi
kuyafanyia kazi maoni ya viongozi wa klabu.
“Viongozi wa klabu wamelalamikia pia mfumo wa tiketi za kieletroniki
na kuweka wazi kwamba mapato yao yameshuka na kufikia asilimia 40,”
alisema Shibo.
Alisema kuwa Bodi ya Ligi imelichukua hilo na kulifanyia kazi na
kueleza kwamba tayari wako katika mazungumzo na kampuni inayohusika na
utengezaji wa tiketi hizo ambao ni benki ya CRDB kwa kushirikiana na
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Kiongozi huyo alimtaja mdhamini
ambaye amepatikana kwenye Ligi Daraja la Kwanza kuwa ni Azam Media ambao
pia wanaidhamini Ligi Kuu.
Katika suala la malalamiko kuhusiana na waamuzi, tayari Kamati ya
Utendaji ya TFF, imeteua kamati maalum ambayo itafuatilia suala hilo na
kutoa maamuzi ndani ya saa 75 baada ya mechi kuchezwa.
Shibo alisema kuwa kamati hiyo itaongozwa na Said Mohamed na Makamu
wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ huku wajumbe ni Charles Ndagala na Steven
Mguto.
Chanzo: NIPASHE
Comments