Skip to main content

Kauli ya JK kwa Polisi inahitaji ufafanuzi

Rais Jakaya Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi nchini kujiandaa kikamilifu kukabiliana na vurugu zozote zitakazojitokeza wakati wa uandikishaji wa wapigakura, upigaji Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa pamoja na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya maofisa warakibu wasaidizi iliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi, Rais Kikwete alisema dalili zinaonyesha kwamba kuna watu wamejipanga wakiwa na nia ya kuhatarisha amani wakati wa matukio hayo.
Kwa tafsiri yoyote ile, kauli hiyo ya Rais Kikwete ni nzito na pengine ndio sababu wananchi wengi waliotupigia simu jana walionyesha hofu kwamba kauli hiyo inahitaji ufafanuzi, vinginevyo inaweza kuchukuliwa na Jeshi la Polisi kama agizo au kisingizio cha kuvunja haki za binadamu kwa kupambana na wananchi iwapo watapinga au kuhoji ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za uendeshaji wa matukio hayo muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu. Hofu hiyo ya wananchi huenda inatokana na maudhui ya kauli hiyo ya Rais, ambayo imeonyesha kwamba Rais amejiridhisha kwamba watu hao ambao hakuwataja wamejipanga kuhatarisha amani wakati matukio hayo yakiendelea.(P.T)
Hoja ya wananchi hapa ni kuwa, kwa kuwa matukio hayo kama Uchaguzi Mkuu na kadhalika ni muhimu sana kwa hali ya baadaye ya nchi yetu, kama kuna watu ambao kweli wamepanga kuvuruga matukio hayo ni lazima wafichuliwe na kudhibitiwa mapema kabla hawajafanikiwa kuvuruga matukio hayo. Hatudhani kama Rais anaweza kutoa tuhuma nzito kama hizo bila serikali yake kuwa na ushahidi wa kutosha wa kuwapo watu hao, ambao bila shaka ni hatari kwa usalama wa nchi yetu. Katika hali kama hiyo, wananchi wako tayari kushirikiana nayo kuhakikisha matukio hayo ya kihistoria yanafanyika kwa amani na mafanikio makubwa. Hivyo, badala ya Rais kuliagiza Jeshi la Polisi nchini kujiandaa kikamilifu kwa mapambano dhidi ya watu hao, tungetarajia watu hao wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kabla ya kutekeleza njama hizo.
Hicho ndicho chanzo cha wananchi kuwa na hofu. Kauli hiyo ya Rais inachukuliwa kama agizo, ambalo uzoefu wetu umetuonyesha kwamba kwa makusudi au kwa bahati mbaya hutekelezwa na vyombo vya dola na mamlaka nyingine za kiserikali kinyume na ilivyokusudiwa. Mara nyingi kauli za viongozi hutekelezwa vibaya kama hazitolewi ufafanuzi wa kutosha. Kwa mfano, kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoitoa mwaka jana kwamba wananchi wasiofuata sheria za nchi 'wapigwe tu' ililichochea Jeshi la Polisi kuzidisha vitendo vya uonevu dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na uvunjaji wa haki za binadamu.
Ndio maana wananchi wanataka ufafanuzi kuhusu kauli hiyo ya Rais Kikwete. Kwamba itakuwapo vurugu, hivyo polisi wajiandae na Serikali itawapa vifaa. Wananchi wanaona kauli hiyo imewaacha njia panda na wanahofia polisi itawaelekezea kipigo, kwani wanatambua kwamba amri ya amiri jeshi mkuu ni amri halali kisheria na kikatiba. Ni amri inayotaka utii wa utekelezaji. Ni amri inayohitaji ufafanuzi, kwani ikitolewa katika nchi kama Tanzania ambayo imekuwa ikiongozwa kwa mujibu wa sheria na Katiba inaweza kutafsiriwa kwamba Jeshi la Polisi halitakuwa na jukumu tena la kulinda haki na usalama wa raia. Kinachotakiwa katika kauli hii ya Rais ni ufafanuzi zaidi.
Chanzo:Mwananchi

Comments