UONGOZI wa klabu ya Simba umeamua kumrejesha kiungo wake, Ramadhani Chombo 'Redondo' na tayari amejiunga na wachezaji wenzake kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo Mbamba Beach, Kigamboni, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Chombo alijiunga na wenzake juzi kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi.
Kamwaga alisema mchezaji huyo amerejeshwa kundini baada ya kuomba radhi kwa uongozi na kusamehewa.
Chombo ni miongoni mwa wachezaji watano wa Simba waliosimamishwa msimu uliopita kwa makosa ya nidhamu. Wengine ni Haruna Moshi 'Boban' na Juma Nyoso waliojiunga na Coastal Union ya Tanga.
Kamwaga alisema kwa sasa Simba inajiandaa kwa mechi moja ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu moja kutoka nje itakayochezwa wakati wa tamasha la Simba Day. Hata hivyo, hakutaja jina la timu hiyo.
Alisema Kocha Abdalla Kibadeni ameomba kambi hiyo ili kuwatengeneza wachezaji kimwili, kiakili na kisaikolojia.
Wakati huo huo, Kamwaga amesema mshambuliaji Kigi Makassy anatarajiwa kwenda India katikati ya mwezi ujao kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya goti.
Kamwaga alisema jana kuwa, uongozi wa Simba umefanikiwa kupata miadi na madaktari wa India kwa ajili ya kumfanyia operesheni mchezaji huyo Agosti 18 mwaka huu.Inatoka kwa mdau.
Comments