Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ametuma ujumbe kwa wale wanaoitishia
Tanzania. Amewaambia wakithubutu watakiona cha mtemakuni kama ilivyokuwa
kwa Idd Amin wa Uganda.
Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakifyatua risasi baridi
hewani kuomboleza vifo vya askari 101 waliofariki katika Vita ya
Ukombozi Msumbiji (1970-1978), wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa
yaliyofanyika Naliendele Mjini Mtwara jana .Picha na Abdallah Bakari
Alisema mamlaka za ulinzi na usalama zilimdhibiti Amin alipofanya
uvamizi katika ardhi ya Tanzania mwaka 1978 na kwamba hazitashindwa
kufanya hivyo kwa mtu mwingine yeyote atakayechezea usalama wa nchi.
Wakati Rais akisema hayo, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange
amewahakikishia wananchi kuwa wakati wote jeshi liko imara na kuwataka
wasiogope lolote.
Viongozi hao walisema hayo jana katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa
iliyofanyika katika Kambi ya Jeshi ya Kaboya iliyopo Muleba, Kagera.
“Sihitaji kusema tena, mmeshamsikia Mkuu wa Majeshi, atakayejaribu
atakiona cha mtemakuni, laleni usingizi na msiwe na wasiwasi,
msisikilize maneno ya mitaani,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Wakati wowote, saa yoyote tuko tayari kulinda nchi yetu. Hatuko tayari
kuona amani inaharibika nchini, hatuwezi kuruhusu mtu yeyote kuimega au
kuichezea nchi yetu kama alivyofanya Idd Amin.”
Katika siku za karibuni kumekuwa na kauli kadhaa kutoka kwa baadhi ya
viongozi wa nchi jirani ambazo zinatafsiriwa na wananchi kwamba ni za
kuitisha Tanzania.
Comments