JIJI la Dar es Salaam leo litakuwa kwenye heka heka kubwa za kumpokea
Rais wa Marekani, Barrack Obama anayetarajia kuwasili saa nane mchana.
Jiji la Dar es Salaam
Ujio wa kiongozi huyo umesababisha kufungwa kwa barabara na kuimarishwa kwa ulinzi katika maeneo mbalimbali.
Kwa takribani wiki moja sasa ulinzi umeendelea kuimarishwa zaidi kwa
kuwashirikisha makachero wa Marekani wakiwemo FBI, CIA na wale wa
Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Obama anayeongozana na familia yake
anatarajiwa kupokelewa jijini Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais
Jakaya Kikwete na baadaye atakwenda Ikulu kwa mazungumzo rasmi.
Taarifa hiyo inabainisha kuwa Obama atapata fursa ya kufanya mkutano na
wafanyabiashara Ikulu pamoja na kuhudhuria dhifa ya kitaifa.
Kesho atakwenda kutembelea mitambo ya kufua umeme ya Symbion iliyopo
Ubungo, Dar es Salaam na kuzindua rasmi Mpango Maalum wa Maendeleo ya
Nishati Barani Afrika ulioanzishwa na Marekani wa Power Africa
Initiative.
Kutokana na ujio huo wa Obama, maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es
Salaam yalikuwa na ulinzi mkali wa makachero wa Marekani na Tanzania
pamoja na barabara atakazopita kiongozi huyo kufanyiwa usafi.
Barabara atakazopita Obama pia zimefanyiwa matengenezo madogo madogo
hususani zile zilizokuwa na mashimo, huku nyingine zikiwekewa taa za
barabarani pamoja na bendera za mataifa hayo mawili.
Comments