Mahakama ya ICC yasikitishwa na Serikali ya Nigeria kushindwa kumkamata al-Bashir licha ya kuombwa kufanya hivyo
Rais Omar al-Bashir akitoka nje ya moja ya hoteli aliyofikia mjini Abuja, Nigeria REUTERS/Afolabi Sotunde |
Na Emmanuel Richard Makundi
Rais wa Sudan Omar al-Bashir ameondoka nchini Nigeria huku mahakama ya
kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC ikitoa hati ya kukamatwa kwa
kiongozi huyo lakini maofisa wa Serikali ya Sudan wamekanusha kiongozi
wao kuondoka kwa kuhofia kukamatwa.
Suala la kiongozi huyo kuwepo nchini Nigeria lilizua hisia kali toka kwa
wanaharakati wa haki za binadamu ambao walikuwa wanaishinikiza Serikali
kumkamata kiongozi huyo anasakwa na mahakama ya ICC kwa makosa ya
uhalifu wa kivita alioufanya nchini mwake.
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC ilitoa taarifa
kudhibitisha kuwa iliiandikia barua Serikali ya Nigeria kutaka vyombo
vya usalama kumkamata kiongozi huyo na kumfikisha kwenye mahakama ya
ICC.
Hapo jana Serikali ya Nigeria kupitia ikulu ya rais Goodluck Jonathan
ilisema haiwezi kumkamata kiongozi huyo kwakuwa hakuja nchini humo kwa
mwaliko wa Serikali bali alienda kwa mwaliko wa Umoja wa Afrika ambao
walikuwa wameandaa mkutano wa afya kwa viongozi wa bara la Afrika.
Comments