ULINZI MKALI KILA KONA, TANZANIA YAKOSOLEWA
HAYAWI hayawi sasa yamekuwa baada ya Rais wa Marekani, Barack Obama,
kuwasili nchini jana kuanza ziara yake ya kiserikali ya siku mbili
akitokea Afrika Kusini.
Rais Obama ambaye alipata mapokezi makubwa ya wananchi na viongozi
mbalimbali, walioongozwa na Rais Jakaya Kikwete, aliwasili katika Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere saa 8:36 akiongozana na mkewe
Michelle pamoja na watoto wao wawili, Sasha na Malia.
Mara baada ya kuteremka kwenye ndege yake ya Air Force One, Rais Obama,
alikumbatiana na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso E. Lenhardt na
mkewe, kisha akasalimiana na mwenyeji wake, Rais Kikwete na Mama Salma.
Rais Obama alikwenda moja kwa moja kwenye jukwaa dogo kisha kupigiwa
nyimbo mbili za Tanzania na Marekani zilizoambatana na mizinga 21, kisha
akakagua gwaride na vikundi vya ngoma za asili.
Huku akishindwa kujizuia kutokana na burudani hiyo, Rais Obama alijikuta
akisakata ngoma na mwenyeji wake, Rais Kikwete na baadaye alisalimiana
na viongozi kadhaa wa kiserikali na mabalozi kisha viongozi hao
walielekea Ikulu kwa mazungumzo.
Wakati wote ulinzi mkali wa maofisa usalama wa Marekani kwa kushirikiana
na wale wa nchini uliimarishwa kila kona, ambako wananchi wengi
walifurika mitaani kumlaki kiongozi huyo.
Baada ya mazungumzo mafupi ya faragha, viongozi hao walikuja mbele ya
waandishi wa habari kwa ajili ya kuulizwa maswali mbalimbali.
Comments