Mwanachama wa Muslim Brotherhood akiwa na picha ya kiongozi aliyeondolewa madarakani Mohammad Morsi REUTERS/Amr Abdallah Dalsh |
Na Flora Martin Mwano
Ofisi ya mwendesha mashtaka nchini Misri imetangaza kuanziasha uchunguzi
dhidi Mohamed Morsi, ambaye ni Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia
na wananchi wa Taifa hilo na kuweka historia ya kukaa madarakani kwa
mwaka mmoja pekee kabla ya kukumbwa na mapinduzi ya kijeshi.
Taarifa ya ofisi hiyo imeeleza kuwa imepokea malalamiko yanayomkabili
Bwana Morsi, wanachama nane wafuasi wa Muslim Brotherhood akiwamo na
kiongozi wa juu katika chama hicho Mohamed Badie.
Malalamiko yanayochunguzwa na ofisi ya mwendesha mashtaka ni pamoja na
uchochezi na kuzorotesha uchumi wa Taifa hilo lililopitia mapinduzi
mengine mwaka 2011 yaliyomuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo
Hosni Mubarak.
Badie pamoja na viongozi wengine wa Muslim Brotherhood tayari
wanakabiliwa na mashtaka mengine dhidi ya uchochezi ingawa hakuna yeyote
kati yao ambaye amekwishakamatwa.
Wakati huo huo wafuasi wa Morsi wameendelea kuandamana kwa zaidi ya juma
moja sasa wakipinga mapinduzi yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo, watu
zaidi ya 90 wanakadiriwa kupoteza maisha katika machafuko yaliyoambatana
na maaandamano hayo.
Marekani na Ujerumani tayari zimetoa wito kwa jeshi kumuachia huru
Morsi, hata hivyo viongozi wa serikali ya mpito wanasema Morsi ambaye
hajaonekana hadharani toka kupinduliwa kwake amehifadhiwa mahali salama.
Via kiswahili.rfi.fr
Comments