Mwenyekiti chama cha wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akilakiwa na wanachama wa chama hicho alipokuwa akiwasili katika ukumbi wa mkutano kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea urais kupitia CUF Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amechukua fomu ya kugombea urais kupitia chama hicho na kuahidi kupambana na rushwa huku akishangaa kuwapo watuhumiwa wa ufisadi waliotakiwa kuwa mahabusu lakini wakichukua fomu za kuwania nafasi hiyo kupitia CCM.
Profesa Lipumba alisema iwapo atapatiwa ridhaa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupeperusha bendera ya umoja huo atahakikisha anaunda Katiba yenye maoni ya wananchi na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuwaunganisha Watanzania dhidi ya ufisadi.
Mwanasiasa huyo mkongwe katika upinzani aliwaambia wafuasi wa CUF waliomsindikiza kuchukua fomu hiyo jijini hapa jana kuwa ameamua kuwania kiti hicho kwa mara ya tano kwa kuwa kati ya viongozi wa juu wa Ukawa anaamini ana sifa, uwezo, uadilifu, uwazi, uwajibikaji wa kuwaunganisha Watanzania ili waondokane na rushwa na ufisadi uliokithiri nchini.
Profesa
Lipumba aliyekabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa CUF Wilaya ya Kinondoni,
Mohamed Mkandu saa 6.55 mchana, alitaja vipaumbele vyake kuwa ni kujenga
misingi ya kuhakikisha watoto wanapata fursa sawa ya maendeleo, ajira,
afya, kulinda rasilimali za umma na kupambana na ufisadi.
Profesa
Lipumba aliyeanza hotuba yake ya takriban dakika 45 kwa kutoa wasifu wa
usomi na kazi mbalimbali za kiuchumi alizozifanya kwa takriban miaka 40,
alisema anafahamu bayana matatizo mengi ya Watanzania kwa kuwa
amezaliwa na kukulia kijijini.
Alisema
matatizo hayo yamesababishwa na “siasa mbovu za chama cha mapinduzi”
ukiwamo ufisadi, hivyo iwapo atapatiwa ridhaa ya kuwania kiti hicho cha
juu, atakuwa na kazi kubwa ya kuleta uongozi makini utakaohakikisha
rasilimali za nchi zinatumika kwa maendeleo ya watu wote.
Alisema
iwapo atachaguliwa kuwa rais, hatakuwa na msalie mtume na mafisadi na
wote wanaohusika watawajibika kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Inatisha
sana kuona mafisadi wakubwa, wala rushwa wakubwa badala ya kuwa ndani
ya jela, wanachukua fomu za urais. Tunahitaji kwa kufuata taratibu na
haki, mafisadi hao watumikie vifungo na mali zilirudishwe kwa umma
walikofisadi,” alisema Profesa Lipumba huku akishangiliwa na wafuasi wa
chama hicho.
Iwapo
atapatiwa nafasi ya urais, alisema katika utawala wake atahakikisha
watoto nchini wanapatiwa fursa sawa ya maendeleo kwa kutoa huduma bora
afya, lishe na elimu.
Alisema
suala la ukuaji imara kwa watoto halijapatiwa kipaumbele na kusababisha
udumavu unaowanyima uwezo mkubwa wa kufikiri pindi wanapokuwa wakubwa.
Kufumua Katiba inayopendezwa
Mwanasiasa
huyo alisema anachukua fomu nchi ikiwa njia panda baada ya Katiba
Inayopendekezwa kuacha masuala ya msingi ya uadilifu na uwajibikaji na
kusababisha wachache kujinufaisha kwa rushwa.
Comments