Chama cha upinzani cha Nigeria kilichoshinda kiti cha urais nchini
humo All Progressive Congress APC kimeanza kukumbwa na mpasuko wa mapema
baada ya kushika hatamu za uongozi kwa muda mfupi.
Mpasuko huo ndani ya APC umejitokeza wakati wa kuwachagua viongozi wa bunge akiwemo spika wa bunge hilo.
Rais Muhamadu Buhari alikuwa amewataka wajumbe wa chama chake
wamchague, Ahmed Lawan kuwa spika wa bunge la Seneti lakini wabunge
walikaidi agizo hilo na kumchagua Bukola Saraki.
Chama kikuu cha upinzani PDP kimetumia vyema mpasuko ndani ya APC na
kufanikiwa kunyakuwa viti kadhaa ndani ya bunge la Seneti ikiwa ni
pamoja na naibu spika pamoja na mratibu wa shughuli za bunge.
Katika hatua nyingine Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari leo anatazamiwa
kuongoza mkutano wa viongozi wa kikanda kujadili juu ya namna ya
kuimarisha mpango wao wa kupambana dhidi ya kundi la kigaidi la Boko
Haram.
Marais kutoka nchi tano za Ukanda huo watashiriki katika mkutano huo utakaofanyika katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.
Mkutano huu wa marais kutoka Niger, Nigeria, Chad, Cameroon na Benin
ulitangulizwa na ule wa Wakuu wa majeshi kutoka mataifa hayo, ambao
Jumatano walikubaliana juu ya mapendekezo kadhaa kuhusu operesheni za
kijeshi kuhakikisha kundi la Boko Haram linatokomezwa.
Kabla ya kuihitimisha ziara yake mjini Paris nchini Ufaransa, rais wa
Benin Thomas boni Yayi, alisema kuwa ana matumaini kuwa juhudi za
pamoja toka mataifa hayo zikiungwa mkono na jumuia ya kimataifa
watafanikiwa kulisambaratisha kundi hilo haramu.
Comments