Alfred Tibaigan
Katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi nyumbani kwake Buganguzi wilayani Muleba, Kamishna Tibaigana alisema suala la maandamano halikumsumbua kwa kuwa alielewa kuwa sheria inayaruhusu, hivyo alichokuwa akifanya ni kuwaita viongozi wa vyama vinavyotaka kuandamana na kufanya nao makubaliano ya namna maandamano hayo yanavyopaswa yafanywe kabla ya kuyaruhusu.
"Pengine hiyo ndiyo sababu sikuwahi kushambuliwa kwa maneno ya kejeli au matusi na wanasiasa kwa kuwa sikuwahi kuzuia maandamano yao bila sababu na hata kama kulikuwa na sababu niliwaita na kuwaeleza na tulikubaliana.
"Kikubwa ni kujenga tabia ya kuwaita viongozi wa waandamanaji na kujadiliana nao, vinginevyo wanaweza pia hata kukufikisha mahakamani wakipinga kuzuiwa maandamano yao," alisema Tibaigana ambaye alikumbana na sakata la kudai maandamano wakati akiwa Kamanda kwenye mikoa ya Tanga, Arusha na Dar es Salaam.(P.T)
"Nilikuwa
nawaita viongozi nakaa nao tunakubaliana. Hata kama ningeambiwa na
kiongozi gani nisitoe kibali, kama hakuna sababu za kweli, nilikataa kwa
kuwa kisheria mimi ndiye nawajibika kama vyama vikishtaki. Ili uzuie
maandamano unapaswa kuwa na sababu za msingi ambazo ukiwaeleza
waandamanaji wanakuelewa."
Tibaigana
anakumbuka jinsi CUF kilivyoandaa maandamano makubwa kushinikiza
kuundwa kwa serikali ya mseto visiwani Zanzibar baada ya kutoridhishwa
na matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2005, lakini anasema kutokana na
msimamo wake, haikuwa vigumu kwake kuruhusu jambo hilo.
"Wakati
wa uongozi wangu CUF ilikuwa na nguvu sana, lakini mimi sikuwa na tatizo
nao. Walipotaka kibali cha kuandamana niliwapa bila woga na tuliishi
vizuri," anaeleza Tibaigana.
Vuguvugu
la maandamano pia lilitanda wakati wa maandalizi ya ziara ya Rais wa
zamani wa Marekani, George Bush nchini kutokana na wasomi na baadhi ya
wanaharakati kutaka kufanya maandamano kupinga vitendo vya taifa hilo
kubwa dhidi ya raia wa Palestina na sehemu nyingine ambako wananchi
wasio na hatia walikuwa wakiuawa.
"Nilichofanya
ni kukutana nao na kuwaeleza njia ambazo wangeweza kutumia katika
maandamano hayo na hali ilikuwa shwari," alisema Kamanda Tibaigana.
Katika
kipindi chake cha uongozi wa Polisi Dar es Salaam, Kamanda Tibaigana pia
alikumbana na vurugu za kidini ambazo zilisababisha askari mmoja
kupoteza maisha, lakini anasema kwa kushirikiana na wadau wengine,
walijipanga na hali ikawa shwari.
Alivyomng'ang'ania Ditopile
Moja ya
matukio makubwa wakati akiwa Kamanda wa Kanda ya Dar es Salaam ni tukio
la mkuu wa zamani wa Mkoa wa Tabora, Ditopile kumuua dereva wa daladala
baada ya kutokea kutoelewana barabarani, hali iliyolazimu sheria kufuata
mkondo wake. Jeshi la Polisi lilitakiwa limkamate mkuu huyo na
kumfikisha mahakamani.
Ditopile
alituhumiwa kufanya mauaji hayo Novemba 5, 2006. Akidaiwa kumuua kwa
kumpiga risasi dereva wa daladala, Hassan Mbonde. Alikamatwa na
kufikishwa mahakamani, lakini alifariki dunia Aprili 20, 2008 wakati
kesi yake ikiendelea.
Chanzo:Mwananchi
Comments