Wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya Wilaya
ya Tunduru mkoani Ruvuma wakiwa wamekaa chini na mwalimu wao pembeni
kuonesha sehemu ambayo hutumika kama darasa wawapo masomoni.
---
Tunduru
WANAFUNZI wa darasa
la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya Wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma wanasomea chini ya mti kutokana na darasa hilo kuendeshwa bila ya
kuwa na chumba maalum kwa ajili ya kusomea wanafunzi hao.
Hali
hiyo imebainika baada ya mwandishi wa habari hizi kuitembelea shule
hiyo hivi karibuni na kuwakuta wanafunzi wakiwa wamekaa chini huku
wakiendelea na masomo hayo nje chini ya mti ulio na kivuli cha
kuwahifadhi wakati wa jua kali.
Akizungumza
shuleni hapo Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nakayaya, Christina
Mhowera alisema watoto hao wamelazimika kusomea nje baada ya huduma ya
elimu hiyo kuanzishwa shuleni hapo bila ya kuwa na jengo maalum kwa
wanafunzi wa awali.
Alisema awali wanafunzi hao
walikuwa wakisomea kwenye gofu (jengo mbovu) lililokuwa jirani na
shule, lakini walilazimika kuondolewa baada ya jengo hilo kutwaliwa kwa
matumizi mengine. Aliongeza kuwa baada ya hapo walihamishiwa kwenye
nyumba ya mwalimu kabla ya kukamilika lakini waliondolewa tena na kuanza
kusomea nje (chini ya mti) hadi sasa.
Alisema
darasa hilo lenye jumla ya wanafunzi 92 linaendeshwa bila ya kuwa na
chumba cha darasa maalum wala madawati kutokana na shule hiyo kukabiliwa
na uhaba wa vyumba vya madarasa hadi hapo watakapopata darasa maalum
kwa ajili ya wanafunzi hao.
Kwa upande wake
mwalimu wa darasa hilo, Teckla Milanzi alisema mbali na darasa hilo
kutokuwa na chumba cha darasa, linakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo
ya uhaba wa vitendea kazi kama vitabu na vyenzo zingine za kufundishia
na hakuna bajeti yoyote inayotumwa kuliwezesha darasa hilo.
Aidha
uchunguzi uliofanywa katika shule nyingine tatu za Wilaya ya Tunduru,
yaani Shule ya Msingi Nanjoka, Majengo na Shule ya Msingi Tunduru
Mchanganyiko kuangalia mazingira ya utoaji elimu ya awali katika shule
hizo umebainisha kukabiliwa na changamoto nyingi hali ambayo
inahatarisha msingi wa elimu kwa wanafunzi.
Kwa
upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nanjoka, Batadhari Mkwela
alisema licha ya usajili wa wanafunzi wa awali kuongezeka kila mwaka
kumekuwa hakuna bajeti ya kuendesha elimu hiyo.
“…Darasa la
awali linahitaji vitendea kazi lakini havipo, hatuna vifaa kama vitabu
vya kutosha, vyenzo za kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa hivi
toka Serikalini, hatuna madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi wa
awali,” alisema Mkwela.
Akizungumzia hali hiyo,
Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, Abdul Kazembe alisema vyumba vya
madarasa ni changamoto kubwa eneo hilo licha ya msisitizo kuendelea
kutolewa wa kila shule ya msingi kuwa na darasa la awali. Alisema mwaka
2013/14 halmashauri ya wilaya hiyo ilihitaji zaidi ya milioni 366.7
lakini ililetewa zaidi ya milioni 196.5 fedha ambayo ni karibia nusu tu
ya kiasi kilichopitishwa kwenye bajeti hiyo.
“…Kwa
hiyo unaweza kuona kwamba ni ngumu kuigawa fedha hii katika matumizi
maana kwanza haitoshi na pili hata kilichotegemewa kuja ni pungufu zaidi
tena sana, sasa sijui unaweza kugawa kila shule ipate shilingi
ngapi…kwani haitoshelezi,” Abdul Kazembe.
Akifafanua
zaidi Kaimu Ofisa Elimu huyo alisema miundombinu ya madarasa ni
changamoto kubwa, kwani mwaka 2013 idadi ya mahitaji ya madarasa kwa
wilaya nzima ilikuwa ni 1,715 lakini madarasa yaliopo ni 900 na kitu
huku mengine yakiwa ni ya muda mrefu na yanaelekea kuchakaa.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
Comments