Zikiwa zimebakia wiki mbili kabla ya kukutana na mahasimu wao wa jadi, Simba imepata pigo kubwa katika timu kwa sababu kipa namba moja wa timu hiyo Ivo Mapunda amevunjika kidole mazoezini Zanzibar jana asubuhi na anatakiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki nane.
Hatoweza kusimama golini wakati tiu yake ikicheza na Yanga October 12 2014 ambapo daktari wa Simba SC Yassin Gembe amesema Ivo aliumia wakati anachupia mpira katika mazoezi ya asubuhi na kwa bahati mbaya mpira ukamgonga kwenye kidole kidogo cha mwisho mkono wa kulia.
Gembe amesema Ivo alitoka mazoezini baada ya tukio hilo na baadaye akapelekwa hospitali ya Mnazi Mmoja kisiwani humo ambako baada ya vipimo ikagundulika amevunjika sana.
“Si kuvunjika kwa mzaha, amevunjika sana na anatakiwa kupumzika kwa wiki nane, baada ya hapo aanze taratibu… ina maana makadirio ya kurudi tena uwanjani ni hadi baada ya miezi mitatu‘ – Gembe.
Kuumia kwa Ivo kunatoa nafasi kwa makipa chipukizi Hussein Sharrif ‘Cassilas’ na Peter Manyika kujibidiisha ili kuziba pengo lake ambapo sasa Ivo anafanya idadi ya wachezaji majeruhi ambao ni tegemeo Simba kufikia wanne baada ya Paul Kiongera anayetakiwa kuwa nje wiki sita, Haroun Chanongo na Issa Rashid ‘Baba Ubaya’.
Comments