Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema hakuna uwezekano wa kubadili muundo wa muungano kutoka Serikali mbili kwenda Serikali tatu katika mchakato wa Katiba.
Kauli ya Balozi Sefue imekuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa Kituo cha Demokrasia (TCD) na kutoa uamuzi wa kuahirisha mchakato wa Katiba hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Suala la
muundo wa muungano lilichukua mjadala mkali ndani ya Bunge Maalumu la
Katiba huku wajumbe wanaounda kundi la Ukawa wakiunga mkono mapendekezo
ya Rasimu ya Katiba ya muundo wa Serikali tatu na wajumbe wa CCM
wakisisitiza muundo wa Serikali mbili.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Balozi Sefue alisema mchakato
wa Katiba unahitaji maridhiano, lakini suala la muundo wa muungano
halina maridhiano katika jamii hivyo litachelewesha upatikanaji wa
Katiba:
"Katika
historia ya nchi yoyote, wakati unafika wananchi wakawa na maridhiano
fulani, wakaamua kuyaingiza ndani ya Katiba. Tatizo linajitokeza pale
watu au makundi fulani yanapong'ang'ania kuingiza ndani ya Katiba mambo
ambayo ni dhahiri hayana maridhiano ndani ya jamii. Mfano ni suala la
muundo wa Muungano," alisema na kuongeza:
"Uzoefu
wa Bunge Maalumu hadi sasa ni kuwa hakuna uwezekano wa kupata maridhiano
ya kubadili muundo wa Muungano kutoka Serikali mbili kwenda tatu.
Hutapata maridhiano hayo ndani ya Bunge Maalumu na hutapata maridhiano
ukienda kwa wananchi," alisema.
Alisema
anaamini wajumbe wa Bunge Maalumu walifanya uamuzi wa busara kuliweka
kando jambo hilo linalotugawa, na kuendelea kujadili Rasimu ya Katiba
kwa msingi wa mfumo uliopo wa Serikali mbili," alisema.
Balozi Sefue aliongeza kuwa tangu suala hilo liwekwe kando kumekuwa na kasi na matumaini ya kupata Katiba Mpya.
Alisema jambo hilo ni kubwa na uzoefu unaonyesha lina uwezo mkubwa wa kutugawa na kuchelewesha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Balozi
Sefue alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliamini yatapatikana
maridhiano kuhusu kubadili muundo wa Muungano, ilivyo sasa, ni wazi kuwa
maridhiano kuhusu mabadiliko hayo hayapo na hayatapatikana.
"Hakuna idadi ya makongamano na maandamano yatakayobadili hali hiyo sasa," alisema.
Licha ya
kusema kuwa kuna matumaini ya kupata Katiba Mpya, Balozi Sefue alisema
ikishindikana Katiba iliyopo itafanyiwa marekebisho ili ituvushe hadi
mchakato utakaporejeshwa tena. (MWANANCHI)
Comments