Rasimu ya Katiba inayopendekezwa imezika rasmi suala la uraia pacha.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mjadala kuhusu uraia pacha, huku
Watanzania wanaoishi nje wakishinikiza kiwepo kipengele kwenye Katiba
kinachoruhusu suala hilo.
Akiwasilisha rasimu hiyo jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa
Katiba, Andrew Chenge, alisema hakutakuwa na uraia pacha isipokuwa watu
wenye asili ya Tanzania ambao hawana uraia watapewa hadhi maalumu.
“Kamati ya Uandishi ilifanya utafiti katika Katiba za nchi nyingine
kama za India na Ethiopia na imebaini wao huwapa watu wenye asili ya
nchi zao hadhi maalumu na kuwawezesha kupata haki mbalimbali,” alisema
Chenge.
Hivyo alisema watu wenye asili ya Tanzania ambao waliacha kuwa raia
wa Tanzania na kupata uraia wa nchi nyingine watatambuliwa na kupewa
hadhi maalumu.
Kwa mujibu wa Chenge, haki hizo ni pamoja na kutohitaji viza za
kuingia na kutoka na kukaa nchini miezi saba bila kuhitaji huduma za
uhamiaji.
Hata hivyo, alisema hawataruhusiwa kupiga kura, kugombea nafasi
yoyote ya kisiasa wala kushika madaraka ya utawala, kumiliki mashamba ya
kilimo au kuwa na makazi.
“Kwa mantiki hiyo, fursa mbalimbali zinazofikiriwa kuwa zitapatikana
kwa kuwapo kwa uraia pacha zinaweza pia kupatikana bila ya kuwapo kwa
uraia pacha,” alisema.
Chanzo: Mtanzania.
Comments