Ukiizumngumzia Yanga ya sasa, lazima umtaje kiungo Mbrazili,
Andrey Coutinho ambaye ni moto kwenye kikosi hicho. Coutinho amewateka
mashabiki wa Yanga pamoja na wa timu pinzani kutokana na juhudi zake
uwanjani ambapo mpaka sasa amecheza mechi nne za kirafiki walizoshinda
dhidi ya Chipukizi bao 1-0, Shangani bao1-0, KMKM mabao 2-0 na Thika
United bao 1-0 zote akafanya vizuri, hajawahi kuwaudhi watu
wanaofuatilia kiwango chake uwanjani.
Mwanaspoti limemfuatilia kwa umakini Coutinho katika mechi hizo na
kugundua mambo makuu matano ambayo ndiyo anayowasumbua nayo wapinzani wa
timu anazokutana nazo.
Anajua kufunga
Katika kikosi cha Mbrazili Marcio Maximo, Coutinho anachezeshwa
pembeni kwenye winga ya kushoto. Pamoja na kuchezeshwa nafasi hiyo ni
hatari sana ndani ya18 kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao tena
kwenye nafasi ngumu.
Anaongoza kwa idadi ya mabao kwenye kikosi cha Yanga baada ya kufunga
mabao mawili sawa na Mbrazili mwenzake, Genilson Santos ‘Jaja’. Mabao
hayo, moja aliwafunga Shangani na lingine KMKM zote za Zanzibar.
Ana nguvu za miguu na anacheza sana na kimahesabu na ni fundi katika
upimaji wa lango pindi anapotaka kufunga. Ni mara chache anapopata
nafasi ya kupiga shuti kisha apaishe au kuutoa nje mpira.
Mipira anayopiga langoni kama haikuwa bao, basi itaokolewa na kipa au mabeki.
Anapotafuta bao, anajua akae eneo gani na kuangalia namna gani atoe
uamuzi sahihi wa kupiga. Coutinho anapokuwa kwenye timu muda wowote
anaweza kubadilisha matokeo ya timu kipaji ambacho ni viungo wachache
wanacho.
Kuchezesha timu
Mbrazili huyo ni mtaalamu wa kuchezesha timu. Pasi zake fupi na
ndefu, zinafika vizuri kwa mtu anayemkusudia. Ikitokea bahati mbaya
mahesabu yake yamekataa na kupoteza mpira, atahakikisha anautafuta kwa
kukaba hadi mwisho, si yule anayekata tamaa mapema.
Anajua kujiweka katika nafasi nzuri na sasa ana uelewano mzuri na
Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, Mrisho Ngassa na Geilson Santos
Santana ‘Jaja’ na wanatengeneza kombinesheni nzuri.
Akili na ujanja
Mhimili mkubwa wa Coutinho awapo uwanjani ni akili, ubongo wake
unafanya kazi na kutoa uamuzi sahihi kwa haraka mno. Anapokuwa na mpira
anajua kujipangia majukumu namna atakavyoutumia na anapokuwa hana,
anaelewa namna gani afanye ili mambo yaende sawa.
Ni mjanja sana jamaa na kwa taarifa, wale jamaa zangu wenye sifa za
kucheza faulo za kijinga, ukimchezea Coutinho anakuumbua. Anapenya sana
uwanjani na anateleza mithili ya nyoka.
Kasi na Wepesi
Kiungo huyu hana mwili mkubwa ni saizi ya kati, lakini ni mwepesi
mno, anaweza kuwa mbele anashambulia baada ya sekunde chache unaweza
kumwona nyuma anazuia. Ana kasi katika kupanda na kuzuia na msumbufu
sana, kama beki anayecheza naye hayuko sawa, anaumbuka.
Mguu wake wa kushoto hatari
Coutinho anatumia miguu yote kucheza, lakini ule wa kushoto ni
hatari. Ndiyo siraha kubwa kwake, shuti lake linalotoka kwenye mguu huo
ni zito. Mabao yake mawili, ameyafunga kwa kutumia mguu huo.
-Makala kutoka Mwanaspoti.co.tz
Comments