Dar es Salaam/Dodoma: Mapendekezo yaliyotolewa katika Rasimu ya Katiba
Mpya na Tume ya Marekebisho ya Katiba yamewavuruga wanasiasa ambao
tayari walikuwa wamejipanga kwa ajili ya kuwania urais katika Uchaguzi
Mkuu wa 2015, Mwananchi limebaini.
Tangu juzi Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba alipotangaza
rasimu hiyo, kumekuwa na wasiwasi mkubwa sasa kwamba mipango ya urais wa
2015 itavurugika ikiwa mapendekezo hayo yatapitishwa.
Tishio kubwa katika rasimu hiyo ni pendekezo la kuwapo kwa Serikali ya
tatu hali ambayo inatafsiriwa na baadhi ya wanasiasa kwamba inaondoa
nguvu ya Rais yeyote; awe wa Jamhuri ya Muungano, Zanzibar au Tanzania
Bara.
Habari za kuaminika zilizopatikana kutoka ndani ya kambi za vyama vya
CCM na Chadema zinaeleza kuwa wale waliokuwa wakifikiria kuwania nafasi
hiyo wameingiwa na wasiwasi.
Kadhalika, suala la umri wa kuwania urais kubakia miaka 40 pia
linaonekana kuwagusa waliowahi kutangaza kutaka nafasi hiyo ya juu ya
uongozi wa nchi kabla ya mapendekezo ya tume.
Katika suala la urais, wanasiasa wenye nia hiyo wanauona uongozi wa
Jamhuri ya Muungano kuwa ni kama hauna nguvu tena kutokana na
kushughulikia mambo machache, lakini wakati huohuo wanauona urais wa
Tanzania Bara kwamba hauna mamlaka kamili ya kuwawezesha watambuliwe nje
ya nchi.
Tume ya Marekebisho ya Katiba imependekeza mambo saba tu yawemo chini ya
Serikali ya Muungano kati ya 22 ya sasa. Yanayopendekezwa ni Ulinzi na
Usalama, Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, mambo ya nje, sarafu
na Benki Kuu, uraia na uhamiaji, usajili wa vyama vya siasa, ushuru wa
bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Muungano.
Comments