WAJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoka Tanzania Bara,
wakiongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, ndiyo
wanaotarajiwa kuandika Katiba ya Tanganyika (Tanzania Bara), vyanzo
kadhaa vya habari vya Raia Mwema vinaeleza.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu ya habari, tayari maandalizi ya muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yamefikia hatua ya kuridhisha na wakati wowote, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema atawasilisha bungeni muswada huo.
Ingawa vyanzo hivyo vya habari vinathibitisha kuwapo kwa maandalizi
hayo, lakini AG Werema hakuweza kupatikana hadi tunakwenda mitamboni,
simu yake ikiita bila kujibiwa.
Tayari Jaji Warioba ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, akihojiwa kupitia kipindi cha televisheni cha Dakika 45
kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, amesema hakuna haja ya
kukusanya upya maoni ya wananchi wa Tanzania Bara kwa kuwa
yamekwishakusanywa na Tume yake na kwamba watakaopewa jukumu la kuandika
Katiba ya Tanzania Bara, wanaweza kutumia maoni yaliyokwishakusanywa.
Lakini wakati hayo yakiendelea, taarifa za uhakika kutoka vyanzo vyetu
vya habari ndani ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CC-CCM)
zinabainisha kwamba kikao hicho kilichoitishwa Jumatatu wiki hii mjini
Dodoma na kuongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete,
kimesikiliza hoja nzito zikiwamo za kuhoji ni wapi Tume ya Warioba
imepata maoni ya kuwapo kwa serikali tatu.
Mjumbe mmoja wa kikao hicho kutoka Zanzibar anaelezea kuchachamaa kwa
wajumbe wa kikao hicho kutoka Zanzibar, wakisema maoni ya Katiba kuhusu
Muungano kutoka visiwani humo yalikuwa ya aina mbili tu na si tatu.
Comments