Na Ali Bilali
Rais Barack Obama wa Marekani anataraji kuipongeza demokrasia iliokita
mizizi nchini Senegal katika duru ya kwanza ya safari yake barani Afrika
ambapo anataraji kutembelea jumba lililotumiwa wakati wa biashara ya
watumwa iliopo kwenye kisiwa cha Goree, ikiwa ni ziara yenye mfano wa
rais wa kwanza mweusi wa Marekani katika kisiswa hicho.
Rais wa Marekani Barack Obama na Macky Sall wa Senegal
derniereminute.sn
Ziara hii ya Obama, barani Afrika itatamatika Julai 3, baada ya
kutembelea nchini Afrika Kusini na Tanzania, hata hivyo, ratiba ya ziara
hii inaweza kupanguliwa iwapo kutatokea taarifa ya kifo cha rais wa
zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela ambaye hali yake imearifiwa kuwa
mbaya zaidi katika saa 48 zilizopita.
Rais Obama amewasili jana Jumatano jijini Dakar akiambatana na mkewe
Michelle pamoja na wanaye Sasha na Malia atakuwa na mazungumzo na
mwenyeji wake Macky Sall alhamisi hii na baadae kuendesha mkutano wa
pamoja na vyombo vya habari.
Wananchi wa Senegal wamejitokeza kwa wingi kumpokea rais Obama na
familia yake ambapo kwenye barabara inayokwenda Ikulu ya rais nyimbo
vificho na nderemo ndivyo vina sikika.
Baada ya mkutano na vyombo vya habari raid Obama atakwenda kukutana na
jaji wa mahakama kuu nchini humo ambako atahutubia kuhusu utawala bora,
ikiwa ni fursa ya kupongeza demokrasia nchini Senegal mtawala wa zamani
wa ukoloni wa Ufaransa iliojipatia uhuru wake mwaka 1960 na ambayo
haijawahi kutokea mapinduzi na ambako marais wamekuwa wakipishana
madarakani kwa amani na utulivu.
Comments